Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mvua zasababisha madhara Dar, wananchi wamwangukia Rais Magufuli

VIDEO: Mvua zasababisha madhara Dar, wananchi wamwangukia Rais Magufuli

Thu, 16 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakazi wa Magomeni na Manzese jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wamemuangukia Rais wa nchi hiyo, John Magufuli wakimuomba aingilie kati ujenzi wa daraja la Jangwani ambalo limekuwa halipitiki wakati wa msimu wa mvua.

Leo Alhamisi Januari 16,2020, Mwananchi imetembelea eneo la Jangwani na kushuhudia daraja likiwa limejaa maji kutokana na mvua kubwa zilizoanza kunyesha alfajiri kiasi cha kuzuia magari na waenda kwa miguu kupita katika eneo hilo.

Katika bonde la Mkwajuni, Kinondoni maji yamejaa na kusabisha magari kutokupita hivyo wananchi kulazimika kushuka katika magari na kuvuka kwa miguu.

Polisi nao wamefunga utepe wa tahadhari kwenye barabara kuzuia magari ya kawaida na mabasi yaendayo haraka kupita katika daraja hilo kwenda maeneo ya Kariakoo au Posta, Dar es Salaam.

Wakizungumza na Mwananchi, wakazi wa Magomeni na Manzese wamesema kufungwa kwa barabara hiyo kunawasababishia usumbufu wanapotaka kwenda kwenye shughuli zao, jambo linalowalazimu kuzunguka umbali mrefu.

"Viongozi wa Serikali wamekuwa wakiahidi kujenga daraja hili tangu mwaka 2011 lakini hatuoni chochote. Tunamuomba Rais Magufuli aingilie kati, tunaona anatekeleza miradi mikubwa, hapa hawezi kushindwa," amesema Ismail Mustapha, mkazi wa Magomeni.

Mkazi mingine wa Magomeni, Said Motisha amesema tatizo la daraja la Jangwani ni kujaa mchanga, jambo linalosababisha maji kushindwa kupita kwa wingi kwa sababu yanakosa nafasi.

"Daraja hili wamelitelekeza kwa muda mrefu, linahitaji kuinuliwa na kuondolewa mchanga uliojaa chini. Zamani maji yalikuwa hayafiki kwenye nyumba za watu kwa sababu mto ulikuwa chini lakini sasa yanajaa majumbani," amesema Motisha.

Kwa upande wake, mkazi wa Manzese, Yusuph Magiza amesema barabara ya Jangwani ni kiungo muhimu kwa wakati za maeneo mbalimbali, hivyo, kufungwa kwake kwa sababu ya mafuriko kunakwamisha shughuli za kiuchumi za wananchi hao.

Chanzo: mwananchi.co.tz