Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mtoto aunguzwa, kisa kucheza kwa jirani

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Rombo. Kucheza kwa jirani kunaweza kuwa kosa? Na kama ikitokea hivyo, adhabu yake ni kuunguzwa miguuni kwa moto?

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mtoto mwenye umri wa miaka minane anayesoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Tarakea, wilayani hapa ambaye ameunguzwa miguuni sehemu za mapaja na shangazi yake kwa sababu ya kwenda kucheza kwa jirani.

Shangazi yake huyo Brigitha Christian Mrosso (26) anashikiliwa na Polisi akidaiwa kufanya tukio hilo mwanzoni mwa mwezi huu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema jana kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake uchunguzi ukikamilika.

Awali, ofisa Tarafa ya Tarakea, Saburi Abdallah alisema baada ya taarifa za mtoto huyo kufika ofisini kwake alifuatilia tukio hilo katika ngazi husika na baada ya kubaini kuwa hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa, aliamua kulisimamia jambo hilo na kumtaka mkuu wa kituo cha polisi kumkamata mara moja.

Anadaiwa kwamba baada ya tukio hilo lililotokea Februari 2, hakumpeleka hospitali, badala yake alichukua maji ya moto na kuyachanganya na sabuni ya unga na kumuogesha mtoto huyo wa kiume.

Jana, mwandishi wetu alikwenda Mbomai, Tarake anakoishi mtoto huyo na kuzungumza naye na kumkuta akiwa hawezi kusimama wala kutembea na akasimulia alichofanyiwa.

“Niliporudi nyumbani shangazi aliniuliza kwa nini nimewaacha watoto wake nikaenda kucheza, ndipo alipoanza kunichoma na kisu cha moto. Baada ya kunichoma, alichukua maji ya moto yaliyochanganywa na sabuni ya omo na kuniwekea kwenye vidonda,” alisema.

Alidai kuwa si mara ya kwanza kufanyiwa ukatili huo na kwamba mwaka jana akiwa darasa la kwanza alichomwa kwenye nyayo kwa kutumia kisu chenye moto, “niliumia sana na nilikuwa nikitembea kwa tabu nilipona japo sikupelekwa hospitali.”

Alivyobainika

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tarakea, Joachim Macha alilieleza Mwananchi jana kuwa mtoto huyo alibainika kuumizwa kutokana na utaratibu waliojiwekea wa kuwakagua wanafunzi na waligundua mtoto huyo amedhoofika hivyo kumuita kujua tatizo linalomkabili.

“Akiwa ofisini kwangu alinifunulia sehemu ya mapaja yake, kukiwa na vidonda vikubwa vya kuungua kwa moto. Alinieleza kachomwa kwa kisu chenye moto mkali na shangazi yake,” alisema.

“Ilibidi niwashirikishe walimu wenzangu ndipo tulipokubaliana twende naye Polisi kutoa taarifa. Polisi waliniambia nimwache watajua cha kufanya. Tuliondoka maana walisema watampigia anayekaa na mtoto huyo.”

Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu tukio hilo, mkurugenzi mtendaji wa shirika la haki za watoto na wanawake (Ajiso), Virignia Silayo alisema ni kitendo ambacho hakipaswi kufumbiwa macho.



Chanzo: mwananchi.co.tz