Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Maofisa ardhi waliofariki ajalini, walifanya kazi siku 192

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Miili nane ya watumishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi waliofariki ajalini imeagwa, huku ikielezwa kuwa walikuwa wamefanya kazi katika ajira zao kwa siku 192 tu.

Pia, Msafiri Kisumo kutoka Shirika la Plan International alifariki dunia kwenye ajali hiyo iliyotokea Jumamosi iliyopita huku wengine wanne wakinusurika baada ya gari aina ya Toyota Land Cruiser (hard top) la halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kutumbukia katika Mto Kikwawila.

Shughuli ya kuaga miili hiyo ilifanyika jana kwenye Uwanja wa CCM Tangani mji mdogo wa Ifakara, Morogoro na kuongozwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula kisha kusafirishwa kwenda kuzikwa makwao katika mikoa tofauti.

Watumishi hao ambao wengi ni vijana walifariki Jumamosi ikiwa ni siku ya 192 sawa na miezi sita tangu walipoajiriwa na wizara hiyo Agosti 15 mwaka jana kwa ajira ya muda kufanya kazi ya Programu ya Uwezeshaji Urasimishaji Ardhi (LTSP).

Mratibu wa LTSP, Godfrey Machabe alizidisha simanzi alipotoa maelezo ya marehemu hao na umri wao.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Rudaya Mwakalebela (25), Sheila Stambuli (32), Maria Kunyanja (25), Shebly Yusufu Shebly (34), Hassan Kayuga (23), Glory Mziray (24), Salome Lukosi (26), Sylivester Mwakalebela (23) na Msafiri Kisumo (46) kutoka Plan International.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk teven Kebwe aliwaomba wananchi kuwa watulivu na kuvitaka vyombo husika kufuatilia kwa makini na kujua chanzo cha ajali na kutenda haki inavyohitajika.

Dk Kebwe alisema vijana hao hakika wataandikwa kwa wino wa dhahabu kwa kukumbukwa kwa namna walivyojitoa katika masuala ya utatuzi wa kero za ardhi.

Alisema Morogoro ni moja ya mikoa inayoongoza kwa migogoro ya ardhi hasa wilaya tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi.

“Vijana hawa wamechangia katika utoaji hati zinazotarajiwa kufikia 300,000 na hadi sasa hati miliki za kimila zilizokamilika ni 280,000 na wao wamekuwa na mchango mkubwa.

Naibu Waziri Mabula alisema Serikali inagharamia mazishi na hadi jana fedha zilizotumika zilikuwa Sh96 milioni kuratibu msiba.

Mabula aliwashukuru wananchi kwa namna walivyojitokeza kusaidia ajali ilipotokea kwani wameonyesha moyo wa upendo.

Alisema Serikali baada ya kuona uwepo wa migogoro ya ardhi ndipo ilipoamua kuleta mradi huo ili kupunguza migogoro hiyo kwa kuanzia katika wilaya hizo za Malinyi, Ulanga na Kilombero kwa imani uwepo wa mradi huo ni suluhisho la migogoro hiyo.

“Vijana hawa walikuwa wakitoka kazini na tuliwategemea pindi watakapomaliza programu hii waende eneo jingine kwa ajili ya utekelezaji,” alisema.

Alisema wizara imesikitishwa na vifo hivyo vya vijana na

wengi walikuwa wasomi wazuri na wangeleta manufaa zaidi kwa

taifa kwa sasa na baadaye.

Naye Katibu mkuu wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika alisema

vijana hao walikuwa hodari na wachapa kazi katika eneo hilo

na kwamba kama wizara wamepoteza nguvu kazi ambayo ilikuwa

tegemezi.

Mwanyika alisema vijana hao waliajiliwa kwa ajili ya

kuongeza nguvu katika mradi huo ili shuhghuli zilizopaswa

kufanywa ziweze kumalizika kwa muda uliopangwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa

alisema, “Lakini kwa maelezo tuliyoyapata kutoka kwa mashuhuda mbalimbali pamoja na majeruhi wametueleza bayana

kuwa dereva tangu mwanzo wa safari yake alikuwa mwendo kasi na ndio uliosababisha ajali hiyo na uhalibifu wa mali ya serikali,” alisema kamanda



Chanzo: mwananchi.co.tz