Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Makonda njia panda

Tue, 24 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Paul Makonda, mmoja wa wakuu wa mikoa vijana nchini ni miongoni mwa viongozi walioanza kwa kasi katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Mipango ya kazi, ufuatiliaji, ujasiri wa kuwataja hadharani waliodaiwa kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni miongoni mwa mambo yaliyoufanya utawala wake utikise.

Miaka miwili ya kwanza tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, mara kwa mara katika mikutano, Makonda alipewa sifa na kiongozi huyo mkuu wa nchi kwa kufanya kazi nzuri na akamtaka ‘asirudi nyuma’.

Lakini, kauli za hivi karibuni za mkuu huyo wa nchi dhidi ya Makonda zinaweza kuwa si ishara nzuri na bila shaka zinamuweka njia panda.

Katika siku za karibuni, Rais Magufuli amekuwa akikosoa hadharani utendaji kazi wa Makonda na viongozi wengine wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Siku mbili zilizopita, Rais Magufuli alieleza kutoridhishwa na utendaji wa Makonda katika utekelezaji wa baadhi ya miradi alipokuwa akiwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Miradi iliyotajwa ni ya machinjio ya Vingunguti na Ufukwe wa Coco (Coco Beach). Rais alisema kuna mkandarasi aliyeshindwa miradi mingine, lakini amepewa wa Coco Beach.

Kuhusu mradi huo alisema, “na ni bilioni 14 lakini mkuu wa mkoa yupo, wakuu wa wilaya kwenye miradi ya Kinondoni wapo, wakurugenzi wapo! Ndiyo ndugu zangu ninazungumza, unapopewa madaraka, lazima uyabebe uwe ‘responsible’ (uwajibike) kwa uchafu utakaotokea,” alisema Rais Magufuli.

Septemba 16, Rais Magufuli alimtaka Makonda ahakikishe miradi hiyo inakamilika kwa wakati kwa sababu tayari fedha zipo.

Siku moja baadaye wakati akizungumza katika hafla ya kuwadhamini wanafunzi wa kike 100 wa kidato cha tano wa masomo ya sayansi ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha, Makonda alisema kama si njaa angejiuzulu ukuu wa mkoa ili kuwajibika.

Pia, Makonda amewahi kukosolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu matumizi ya shisha katika mkoa wa Dar es Salaam pia Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amekuwa mara kwa mara akisema mkuu huyo wa mkoa anapaswa kuwekwa katika orodha ya viongozi vijana wanaotakiwa kupewa mafunzo.

Pamoja na kupitia katika changamoto hizo, Profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Iringa, Gaudence Mpangala anaona bado Rais Magufuli anamhitaji Makonda.

“Haina maana kuwa atatengua uteuzi wake, anamkemea ili ajisahihishe. Kama kumtumbua angeshamwondoa siku nyingi. Yeye mwenyewe yuko kwenye harakati za kujirekebisha ili aendane na maoni ya Rais,” alisema.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohamed Bakari alisema viongozi wa manispaa, halmashauri hadi ngazi za chini wanapaswa kuweka utaratibu unaoeleweka ili mipango ikamilishwe.

“Mkuu wa mkoa ni msimamizi. Yeye si mtekelezaji, katika Serikali kuna bajeti zake pale anaangalia mambo yanafanywa namna gani, unapomlaumu sioni kama ni sawa kwani Serikali za mitaa pamoja na rasilimali chache walizonazo wanapaswa kusimamia mipango yao ikamilike kama ilivyopangwa,” alisema.

Alisema kuna miradi mikubwa haiwezi kusimamiwa na jiji au manispaa ila inafadhiliwa fedha nyingi na Serikali Kuu. “Tunaona hivi sasa ni Dodoma pekee ndiko kuna miradi mingi inaenda vizuri na kwa kuwa inafanywa na Serikali Kuu,” alisema Profesa Bakari.

Pia, wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema jiji la Dar es Salaam lina kazi nyingi ambazo zipo chini ya manispaa na mkuu wa mkoa si muwajibikaji wa moja kwa moja.

“Huko kuna meya na mkurugenzi halafu kuna jiji, sioni kama Makonda ameshindwa kufanya kazi isipokuwa kuna watendaji wanamwangusha, kinachopaswa hapa awe mkali kwa watendaji wa chini, mfano machinjio ya Vingunguti yanasimamiwa na manispaa na ndivyo ilivyo kwa Ufukwe wa Coco.”

Matukio ya nyuma

Machi 2017, Makonda alitajwa kuvamia studio za Clouds Media Dar es Salaam na kudaiwa kuwalazimisha watangazaji wa kipindi cha Shilawadu kutangaza kipindi kilichokataliwa na uongozi wa televisheni hiyo.

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye aliunda kamati kuchunguza tukio hilo ikiwamo kumhoji Makonda, lakini mbunge huyo wa Mtama alipoteza uwaziri.

Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa barabara za juu (flyovers) Ubungo, Machi 20, 2017, Rais Magufuli alisema, “Mimi ndio najua nani anatakiwa kuwa wapi akae wapi, ni mimi ninayepanga. Kwa hiyo Makonda wewe chapakazi, nasema chapa kazi.”

Akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 33 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat), uliofanyika Oktoba 4, Rais Magufuli alimtolea mfano wa kuigwa Makonda kwa wakuu wote wa mikoa kwa kubuni mbinu za kutafuta fedha na misaada itakayosaidia maendeleo. “Hata kama hajui ‘A’ kama, anakamata wauza dawa kwangu naona ni mzuri, tatizo si vyeti ila tunaangalia uzalendo, wasomi ndio wametuangusha,” alisema Rais.

Agosti 27, mwaka jana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alimshukia Makonda kuhusu sakata la mnada wa makontena 20 yaliyokuwa bandarini. Makontena hayo yaliyokuwa na samani za ndani kama viti, meza na mbao za kuandikia yenye umiliki wa Makonda yalikuwa yakidaiwa kodi inayokadiriwa kufikia Sh1.2 bilioni.

Baada ya Makonda kutaka yasiguswe, Dk Mpango aliibuka akiwaonya viongozi serikalini kuchunga maneno yao na kuwaomba wanaotaka kununua samani hizo wasiogope.

Majaliwa aliwahi kumuonya

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alishamwonya Makonda mwaka 2016 wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme jiji la Dar es Salaam, akisema atamwajibisha iwapo hatasimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya dawa za kulevya aina ya shisha.

Chanzo: mwananchi.co.tz