Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Makonda awashukia waajiri Dar

Video Archive
Fri, 21 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema waajiri wote walioajri wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha asilimia tatu ya wafanyakazi hao ni walemavu.

Makonda amesema hayo leo Alhamisi Septemba 20, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake.

Amewaomba waajiri kufuata matakwa ya Sheria ya watu wenye ulemavu namba 9 ya mwaka 2010 kifungu cha 31 inayomtaka kila mwajiri aliyeajiri wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha asilimia tatu ni walemavu.

Amesema ajira kwa walemavu inakabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na waajiri kutokuwa tayari kuwaajiri au kutoa fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo.

"Nawapata muda kuanzia mwezi huu hadi Januari mwakani kila kampuni iwe kwenye sekta binafsi au ya umma iliyopo kwenye mkoa huu iwe imeajiri kulingana na matakwa ya Sheria ya watu wenye ulemavu,” amesema.

"Ikifika Januari mwakani tutafanya ukaguzi kwenye kampuni ili kubaini kama hilo limefanyika.”

Makonda amefafanua kuwa mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu kifungu cha 27 unazitaka nchi wanachama kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa fursa sawa ya ajira pasipo ubaguzi kwa misingi ya ulemavu wao.

Naye meneja wa kitengo cha utetezi na ushawishi wa masuala ya watu wenye ulemavu kutoka Hospitali ya CCBRT,  Fredrick Msigalah ameiomba Serikali kuweka mkakati wa makusudi na kufuatilia utekekezaji wa sheria na mikataba inayolinda ajira kwa watu wenye ulemavu.

Amesema waajiri pia wanapaswa kulizingatia hilo kwa kuweka mazingira rafiki kwa walemavu katika maeneo yao ya kazi ili kuwawezesha kufanya kazi bila shida.

"Tunawaomba waajiri wawatumie wataalamu wa masuala ya walemavu kutoka CCBRT kupata mafunzo ya namna ya kuwajumuisha watu wenye ulemavu,"amesema Msigalah.

Amesema CCBRT kuna dawati linaloshughulikia ajira kwa walemavu lenye kanzi data ya walemavu wanaotafuta ajira.

"Kwenye kanzi data kuna wataalamu wa fani mbalimbali wakiwamo wasomi wa stashahada na astashahada," amesema Msigalah.

Chanzo: mwananchi.co.tz