Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kudai anahujumiwa na baadhi ya watendaji wake wa chini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wadau mbalimbali wamesema kiongozi huyo anaweza kuwa anajihujumu mwenyewe.
“Anahujumiwa yeye akiwa wapi? Huwezi ukasema hadharani unahujumiwa, una watendaji wako na wewe ndio msimamizi wao. Unapokuwa msimamizi ukiona wale unaowasimamia hawafanyi unavyotaka una njia za kuwaelekeza na kuwawajibisha na siyo kulalamika,” alisema mkurugenzi wa zamani wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo- Bisimba.
Juzi katika kikao na watendaji wa wilaya, ikiwa ni siku mbili baada ya Rais John Magufuli kuonyesha kutoridhishwa na ufuatiliaji wake wa miradi ya maendeleo, Makonda alisema baadhi ya watendaji wamemchongea na ili kazi ziende ameamua kuanza kuzunguka na maofisa wa Jeshi la Polisi katika miradi hiyo ili anapokuta mambo hayaendi arudie tena mtindo wa kuwaweka mbaroni.
Dk Helen alisema “huu sio uongozi, kiongozi ndiye msimamizi wa kila kitu katika timu yako unamjua kila mmoja. Ukimuona huyu hapa mcheleweshaji wa mambo, unajua nini cha kufanya au huyu nikimwambia aende hivi lakini yeye anakwenda vile unajua cha kumfanya.”
Dk Bisimba alisema kiongozi hawezi akatoka mbele za watu na kulalamikia watendaji wake, wakati ndiye msimamizi wao, “nadhani mambo ya kiutalawa yamempiga chenga mkuu huyu wa mkoa.”
“Ukiwa kiongozi ndiyo nafasi yako ya kuwasaidia unaowangoza.Kama wanakuhujumu na umebaini unawachukulia hatua za kuwashughulikia kabla mambo hayajaenda mbali, hapaswi kulalamika kama ana hujumiwa, kama wapo awashughulikie,” alisema Dk Bisimba.
Habari zinazohusiana na hii
Kauli ya Dk Helen iliungwa mkono na mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga aliyesema kiongozi kama haeleweki ajue ana matatizo, kwa sababu kiongozi mahiri ni yule anayejenga timu yake pamoja, kwa kuelewa maono ya ofisi husika.“Kiongozi yeyote lazima uhakikishe unawasiliana na wenzako kuhusu maono ya ofisi yako. Kila ofisi ina maono yake, kuna maono ya wizara, mkoa na wilaya au halmashauri, kiongozi anatakiwa mara kwa mara afanye mawasiliano na kuonyesha kwa vitendo na kuyasimamia,” alisema Henga.
“Ikifikia hatua kiongozi anasema anahujumiwa ujue kuna udhaifu kwenye uongozi wake na kujenga timu yake. Inawezekana kweli wanamhujumu, lakini hawajaelewa wanakwenda wapi? Kiongozi ukikimbia mbele na kuwaacha watu nyuma, lazima watakatisha njia na wengine kurubuniwa,”alisema.
“Sijajua kwa nini amezungumza sasa hivi kauli hii, lakini Dar es Salaam kuna matatizo mengi na Rais Magufuli aliyasema na Makonda ndiye anayewajibika. Inawezekana anajitetea, ili aonekane anaweza, lakini watendaji wake wanamuangusha, ila kiongozi ndiye anayelaumiwa na siyo watu wa chini,” alisema.
Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema Dar es Salaam kuna kazi nyingi ikiwemo miradi ya maendeleo na mkuu wa mkoa Makonda hana mamlaka ya moja kwa moja ya kuhusika isipokuwa kuisimamia na kutoa ushauri.
Dk Kyauke alisema mkuu wa mkoa hahusiki kwenye mchakato wa zabuni au kumtafuta mkandarasi na hana nguvu za kumchukulia hatua mtendaji wa chini kwa sababu asilimia kubwa ni wateule wa Rais Magufuli.
“Ni kweli anaweza kutoa maelekezo na yasitekelezwe na watendaji wa chini, anaweza akamuagiza mkurugenzi kufanya jambo fulani na asilifanye. Sheria haimpi mamlaka ya kuteua na kuwawajibisha watendaji.
“Ameamua kuzungumzia haya baada ya kuona maelekezo yake hayafanyiwi kazi ipasavyo. Pia amezungumza baada ya kubanwa na kiongozi wake wa juu, kiongozi wa juu akikubana lazima wewe uwabane wa chini yako,” alisema Dk Kyauke.
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema kinachotokea sasa ni dalili za mwisho za Makonda kwenye zama za utendaji kazi wake. “Kitendo cha Rais Magufuli kumkosoa hadharani ni dalili ameanza kumchoka. Kukosolewa kwake hakuhusiani na vimemo vya watendaji wake, bali makosa yake yapo dhahiri na kila mtu anayaona,” alisema Shaibu.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alisema kumekuwa na tabia ya viongozi kulalamika na ameuita huo kuwa ni udhaifu kwa Taifa kwa sababu wanatakiwa kuchukua hatua.
“Unaposema mtu anakuhujumu nashindwa kuelewa, hivi anakuhujumu kwa misingi gani? Ukishakuwa kiongozi unapaswa kusimamia kazi zilizopo kwa mujibu wa sheria na ukiona mtendaji hafuati utaratibu wako unamuwajibisha,” alisema Ole Ngurumwa.
Alisema kiongozi hapaswi kulalamika kwa sababu ana mamlaka, ila anaweza kutoa malalamiko endapo atafanya mambo ambayo hayapo katika mfumo wake ikiwemo kuongeza majukumu na mamlaka yasiyo ya kwake.