Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Kwa kasi hii, DC Kilolo mtegoni

Video Archive
Mon, 30 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama ile kasi ya ‘ukiibua-natimua’ ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa iliyoonekana kwa watumishi mkoani Morogoro itaendelea, basi mkuu wa wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah hana budi kuwa na wasiwasi--angalau kwa sasa.

Mkoani Morogoro, Majaliwa alieleza udhaifu wa watumishi wa Serikali mkoani na wilayani, na siku moja baadaye Rais Magufuli alitengua uteuzi wa watumishi waliotajwa na Waziri Mkuu.

Juzi Majaliwa hakumuonea aibu mkuu wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdalah alipomsema hadharani kwa kutumia madaraka yake vibaya na kutokuwa na uhusiano mzuri na watumishi wa ofisi yake.

Waziri Mkuu alisema mkuu huyo amekuwa hana maelewano mazuri na watumishi wake jambo linalofanya baadhi yao kuogopa na kukosa raha huku baadhi wakiamua kuomba kuhamia wilaya nyingine na hata waliopo hawataki kuendelea kufanya naye kazi.

Hadi sasa tangu kuteuliwa kwake mwaka 2016 ameshabadilisha madereva tisa na aliyenaye ni wa 10 pia wasaidizi wake, Hilda Mtumle, ambaye ni katibu tawala, Upendo Mtaki (katibu muhtasi) na Goodlove Gama (mtunza kumbukumbu) wamewahi kuwekwa ndani saa 24.

Pengine Asia anaweza kujifariji kwa kauli ya Waziri Mkuu kutaka mkuu wake wa mkoa amuulize anataka dereva gani, kitu kinachoweza kueleza kuwa uteuzi wake hauwezi kutenguliwa katika siku za karibuni.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Lakini bado wachambuzi wanaona bado mkuu huyo wa Kilolo hajafanya vizuri.

“Huo ni uongozi wa kibabe na kutumia mamlaka zaidi bila busara. Hata madereva tu unabadilisha wanafika 10? Mimi nahisi kuna tatizo fulani katika sehemu hizi,” alisema Dk Richard Mbunda ambaye ni mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema viongozi wengi wanapoteuliwa huhisi kuwa na haki na madaraka hata ya kuwaweka ndani watu kwa saa 24 na kwamba yote hayo hutokea kutokana na kukosekana kwa semina elekezi kwa viongozi.

“Wangepewa ile semina wangekuwa wakijua nini wanapaswa kufanya katika nafasi zao na hapo wangejikuta wanatumia nguvu nyingi kusukuma maendeleo badala ya kusukuma watu kama hivi sasa,” alisema Dk Mbunda

Lakini licha ya kunyooshewa kidole na Waziri mkuu, Dk Mbunda alisema huenda mkuu huyo wa wilaya akasalia katika nafasi yake kwa kuwa wapo baadhi ya viongozi waliowahi kusemwa na hawajatolewa.

“Lakini jibu si kubadilisha na kuleta mwingine. Anaweza kuja hali ikawa ileile kwa sababu hawana semina elekezi na maamuzi ya Rais hayatabiriki. Anaweza kusemwa na asitolewe na tumeshuhudia wengine ikiwa hivyo,” alisema Dk Mbunda.

Profesa wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Iringa, Gaudence Mpangala alisema huenda kinachofanywa na mkuu wa wilaya ya Kilolo ni kama anaiga, kuiga bila kujua kuwa kila ngazi ina majukumu yake.

“Labda ana hulka ya kutovumilia watendaji wake wa chini jambo ambalo ni tatizo. Anatakiwa kuvumilia, kuwaelekeza na kabla ya kuwaondoa anatakiwa kuwapa onyo kwanza,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz