Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Jokate akabidhiwa mzigo wa majukumu ya Kisarawe akiapa

Video Archive
Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Mkuu mpya wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo ameapishwa jana huku akitwishwa mzigo wa majukumu atakayokabiliana nayo katika kipindi cha uongozi wake.

Miongoni mwa majukumu hayo ni kuongeza kasi ya uanzishaji viwanda na uwekezaji mkoani humo, usalama wa bandari na ukusanyaji wa mapato.

Pamoja na Jokate, mwingine aliyeapishwa jana na kupewa majukumu kama ya Jokate ni Zainab Kawawa, Mkuu wa Wilaya Bagamoyo.

Zainab na Jokate waliteuliwa Julai 28 na Rais John Magufuli. Pia Rais aliteua wakuu wa mikoa, makatibu wakuu, manaibu katibu wakuu na makatibu tawala wa mikoa.

Pamoja na hao, wakuu wapya wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam (Kigamboni na Kinondoni), Sara Msafiri na Daniel Chongolo walikutana jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika hafla ya ukaribisho.

Jokate ambaye aliwahi kuwa mshindi wa pili katika mashindano ya Miss Tanzania 2006 alipewa majukumu hayo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha, Ndikilo aliwataka wawe wasimamizi wa Serikali wilayani humo.

“Wewe ni kiongozi na msimamizi wa Serikali ndani ya wilaya yako, hakuna jambo ambalo halikuhusu katike eneo lako,” alisema.

Pia, aliwataka kuwa tayari kila wakati kutoa ufafanuzi wa kina wa suala lolote ndani ya wilaya zao. Mengine ni kusimamia Katiba na kusikiliza matatizo ya wananchi.

Majukumu mengine waliyopewa wakuu hao wa wilaya ni kusimamia sekta ya kilimo na uvuvi.

“Hakikisheni mnakusanya mapato ya ndani kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali na isiwe chini ya hapo,” alisema.

Ndikilo pia alisisitiza suala la uwekezaji wa viwanda na kuwataka kutengeneza mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji.

“Kwa Bagamoyo, DC Zainab huko kuna uwekezaji kiwanda cha sukari cha Bagamoyo wanataka ikifika 2020 wawe na kiwanda tayari hapo, kakae na watendaji wako ili muwekezaji huyu atekeleze hilo,” alisema.

Pia aliwataka wakuu hao wa wilaya kuzingatia suala la usalama wa Bandari ya Bagamoyo.

“Pia kuna bandari ambapo vifaa vya magendo vinapitishwa huko nalo ukalisimamie sana kakae vizuri na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na Polisi haiwezekani kupitishwa magendo hapo na kuipotezea Serikali mapato,” alisema.

Jukumu jingine walilopewa ni kuhakikisha wanakuwa na kamati za amani za wilaya na wawe na ushirikiano nazo.

Pia, wametakiwa kusimamia ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kilimo, kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ili yasitokee mapigano.

“Kuna hili la uharibifu wa misitu, Kisarawe upo msitu wa Kazimzumbwi, Jokate akausimamie, Ruvu Kusini kwa Bagamoto isivamiwe na kuwepo na maelewano ya ndani ya maeneo ya kiutawala,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zainab Vullu alitaja sababu za Rais Magufuli kumteua Jokate.

Alisema kilichomfanya aaminiwe ni uchapakazi wake, elimu na uadilifu.

Alimtaka Jokate kuhakikisha anayatimiza yale yote aliyoahidi kwenye kiapo na asimuangushe Rais kwa kuwa amemuamini na kumpa wadhifa huo wa uongozi.

“Yaliyopita si ndwele tugange yajao. Jokate mengi yamesemwa lakini ninachoweza kuueleza umma huu wa Pwani ni kwamba kilichokufanya uaminiwe na Rais ni uadilifu wako, uchapakazi na elimu, hivyo kachape kazi usimuangushe Rais,” alisema.

Vullu aliwataka wateule hao wasiende kufanya jambo kwa utashi wa mtu, bali wakatekeleze yale yanayofaa.

“Msibabaike wala msitetereke, chapeni kazi jamani na msisite kushirikiana na sisi wabunge tupo,” alisema.

Makonda ataka uhakiki wa mali za Serikali

Wakati Jokate na Zainabu wakipewa maagizo hayo, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemwagiza katibu tawala wa mkoa huo, Abubakar Kunenge kufanya uhakiki wa mali za Serikali ndani ya mwezi mmoja.

Sambamba na agizo hilo, amemtaka kusimamia kwa karibu maeneo manne muhimu kwenye mkoa huo ambayo ni ardhi, biashara, usafi na michezo pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato.

Makonda alitoa maagizo hayo jana kwenye hafla ya kumkaribisha Kunenge pamoja na wakuu wapya wa wilaya, Daniel Chongolo (Kinondoni) na Sara Msafiri (Kigamboni).

Pia, kwenye hafla hiyo, waliokuwa wakuu wa wilaya hizo waliagwa akiwamo Ally Hapi ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa na aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashimu Mgandilwa ambaye sasa amehamishiwa Wilaya ya Ruangwa.

Alimtaka Kunenge kuunda timu yake na kuandaa ripoti maalumu ambayo inaeleza mali zilizopo katika mkoa huo na namna zinavyotumika. Alisema anazo taarifa kwamba viwanja vingi vya Serikali vimechukuliwa na watu binafsi.

“Nakutaka utengeneze timu yako ndani ya mwezi mmoja tupate ripoti, Dar es Salaam manispaa zina viwanja kiasi gani, nyumba ngapi na zinatumikaje,” alisema Makonda.

Kuhusu biashara, Makonda alisema kuna haja ya kutengeneza mfumo mbadala ambao utawarahisishia kazi wafanyabiashara.

Alisema mfumo huo unaweza kuwa kituo cha pamoja cha huduma (one stop centre) katika mkoa huo ili vibali vyote vipatikane sehemu moja na kwa haraka.

Kuhusu suala la ukusanyaji wa mapato, Makonda alimwagiza katibu tawala kukutana na wakurugenzi wa halmashauri zote za Dar es Salaam kujadiliana kwa nini wamepitwa na Dodoma katika ukusanyaji wa mapato na kutafuta suluhisho lake.

Imeandikwa na Julieth Ngarabali, Peter Elias, Rhobi Chacha na Peter Edson.

Chanzo: mwananchi.co.tz