Hajawa na jina kubwa katika uga wa fasihi nchini, lakini huwezi kuamini kuwa ana vitabu vinavyotumika kufundishia wanafunzi katika ngazi ya chuo kikuu.
Huyu ni Ismail Himu, ambaye katika umri wa miaka 32, tayari ameshaandika vitabu kadhaa vya fasihi, vikiwamo viwili vinavyotumika vyuoni.
Anasema haikuwa safari rahisi kufika hapo hasa katika jamii ya Kitanzania na mfumo wa elimu ambavyo bado vinawakumbatia watunzi wenye majina makubwa. .
Ni kwa sababu hiyo, hata alipotoa kitabui chake cha kwanza alichokipa jina la ‘Chanzo ni Wewe’ aliishia kukiuza kwa watu wachache kutokana na kukosa ithibati kutoka kwa mamlaka husika.
Anasema masharti magumu wanayowekewa watunzi wanaochipukia huchangia kuwakatisha tamaa, hivyo majina ya waandishi wakongwe kuendelea kusikika.
“Ukweli ni kwamba kuna vijana wengi wanapenda kuandika na wana uwezo wa kuandika vitabu vizuri lakini mchakato wa kukifanya hicho kitabu kiwafikie watu ndio unaowakatisha tamaa,” anasema.
“Unaambiwa muswada wa kitabu ili upitiwe unatakiwa ulipe Sh500, 000 baada ya kitabu kinatakiwa kufanyiwa uhariri na kuangaliwa kama kinaweza kutumika shuleni kwa Sh1.3 milioni unafikiri kwa mwandishi chipukizi anawezaje gharama zote hizi?’’
Anasema kutokana na hilo hata wanafunzi ambao ndio watumiaji wakubwa wa vitabu shuleni wanaishia kusoma vitu ambavyo haviendani na mazingira ya sasa ambavyo ndivyo vinavyondikwa na waandishi wanaochipukia.
Himu anaeleza kuwa mabadiliko ya nyakati yanapaswa kwenda sambamba na vitabu vinavyoandikwa na kutumika shuleni, ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza vitu ambavyo vipo kwenye mazingira yao kwa wakati huo.
Anabainisha kuwa soko kubwa la vitabu linalotegemewa na waandishi kama yeye ni taasisi za kielimu hususan shule za msingi na sekondari, iikiwa vitabu vya waandishi wakongwe ndivyo pekee vitakavyotumika anasema kuna hatari ya waandishi chipukizi kukata tamaa.
“Haina maana kwamba waandishi wa zamani hawafahi ila ni muhimu na vitabu vinavyoandikwa na waandishi vijana navyo vikapewa nafasi kwa sababu wanaandika mambo yaliyopo sasa,” anaeleza.
Ukimwambia mwanafunzi wa sasa kuhusu uhujumu uchumi anaweza asielewe lakini ukimtajia ufisadi atajua ni kitu gani unamaanisha.”
Himu ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma anaongeza: ‘’Mtu amesoma kitabu cha Ngoswe sekondari, kitabu hichohicho akakisoma chuo, ni wazi kwamba atachoka na hata uelewa wake utabaki kuwa uleule. Inafikia mtu maisha yake yote amesoma kitabu hicho tu”
Anasema urasimu huo umekwenda hadi kwenye soko la kimataifa, ambapo waandishi wanashindwa kufikia soko hilo na kutambulisha vitabu vyao. Matokeo yake vitabu vya wakongwe ndio vinavyoendelea kutumika hata nje.
Licha ya kusomea fani ya Jiografia na mazingira chuoni, Himu ameamua kujikita katika uandishi wa vitavu vya fasihi, shauku anayosema alianza kuvutiwa nayo tangu akiwa sekondari.
Anasema wakati huo alivutiwa na kazi mbalimbali za watunzi wa fasihi na kujikuta akitamani kujitosa kwenye fani hiyo inayohitaji umakini kupita kiasi.
Anasema siku zote amekuwa akiangalia kazi za mwandishi mahiri wa vitabu Shaban Robert na kutaka kufuata nyayo za gwiji huyo anayetajwa kuwa miongoni mwa watunzi nguli wa fasihi.