Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Familia mwanafunzi aliyejinyonga yamgeukia mkuu wa shule

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Familia ya aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika Sekondari ya Rau iliyopo mjini Moshi, Emmanuel Tarimo (18) aliyejinyonga, wamemlalamikia mkuu wa shule hiyo, Nyoni Njinjinji wakidai amewatolea maneno yasiyo na staha.

Wanafamilia hao walifika shuleni hapo jana mchana kwa lengo la kuhoji ni kwa nini walimu walichukua jukumu la kumhoji mwanafunzi huyo bila wazazi kupatiwa taarifa.

Dada wa Emmanuel, Teddy Maro alidai baada ya kufika kwa mkuu huyo wa shule hakuonyesha ushirikiano kwao, badala yake walipewa vitisho. Alisema mwalimu huyo aliwatishia akisema atawaitia polisi ili wakamatwe.

“Inasikitisha sana sisi tunauliza sababu (za kufanya hivyo) yeye anatujibu eti suala la kuhojiwa kwa mwanafunzi halituhusu, hii siyo haki. Sisi tulitaka kujua walimuuliza nini mtoto hadi akafikia hatua ya kujiua,” alisema Teddy. Alisema, “na mbaya zaidi hadi sasa hivi (muda wa mchana jana), hakuna mwalimu hata mmoja aliyefika msibani.”

Babu wa mwanafunzi huyo, Jerome Maro alisema hawakuridhishwa na kitendo cha mwalimu huyo kuwafukuza ofisini kwake, hivyo wanafikiria kufungua kesi kulalamikia kifo cha mjukuu wake.

“Tunaiomba Serikali ishughulikie jambo hili, kifo cha mtoto wetu kina utata na kwa nini mtoto baada ya kuhojiwa tu shuleni aliporejea nyumbani akajiua?” alihoji Maro.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi, mkuu wa shule, Njinjinji alihoji ushirikiano gani wanaotaka ndugu hao kutoka kwake.

“Sisi kama ilivyo kawaida tutatoa rambirambi kama tunavyofanya kwenye misiba mingine inayotokea shuleni hapa na Emmnuel si mwanafunzi wa kwanza kufariki dunia, hivyo tutaoa rambirambi kama tunavyofanya kwa wengine,” alisema.

Taarifa ya polisi

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah ilisema hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na kifo cha mwanafunzi huyo.

Emmanuel alikutwa amejinyonga hadi kufa kwenye sebule ya nyumba yao usiku wa kuamkia Septemba 4, kwa kutumia mkanda wa suruali baada ya kutuhumiwa kumpa mimba mwanafunzi mwenzake anayesoma kidato cha kwanza. Atazikwa kesho kijijini kwao Mashati Rombo.

Chanzo: mwananchi.co.tz