Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) Cyprian Luhemeja amesema shida ya maji kwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani inakwenda kuisha baada ya kusaini kwa mikataba sita ya maji itakayoboresha huduma hiyo.
Luhemeja ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Julai 2, 2019 wakati wa hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya Dawasa Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, naibu wake, Jumaa Aweso, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.
Luhemeja amesema mikataba hiyo ina thamani ya zaidi ya Sh114 bilioni kati ya hizo Benki ya Dunia (WB) imefadhili kwa kutoa Sh77 bilioni zilizobaki ni fedha za ndani za mamlaka hiyo.
“Kwa mikataba hii tunayoisaini leo mheshimiwa waziri ikisimamiwa vyema changamoto ya maji katika jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani itaisha,” amesema Luhemeja.
Amesema Sh77 bilioni zitakwenda kuboresha huduma ya maji maeneo ya Salasala, Bunju, Wazo, Changanyikeni, Bagamoyo, Kibaha, Kibamba, Kiluvya, Mbezi mwisho, Msakuzi, Vikawe pamoja na maeneo yote ya Dar es Salaam.
“Pia yataboresha huduma ya maji maeneo ya Yombo, Buza, Tandika na Mwagati. Mradi huu utahusisha utandazaji wa bomba la urefu wa kilomita 1426, ujenzi wa matenki matano yenye ujazo wa mita milioni sita eneo la Malamba mawili, Msakuzi, Goba, Mbweni na Madale,” amesema Luhemeja.
Pia Soma
- Majina ya wakandarasi, wahandisi wababaisha sekta ya maji kutajwa
- Msichana wa kazi anayedaiwa kuiba mtoto wa siku moja adakwa
- MAAJABU: Afunga ndoa na Mamba
Luhemeja amefafanua tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015b Dawasa hawajawahi kupandisha ankara ya maji na hawana mpango huo badala yake itaendelea kuunganishia maji wateja wake kwa mfumo wa mkopo.
Miradi hiyo ambayo imeainiwa ni wa usambazaji maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo; Mradi wa bomba la kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza; mradi wa kuendeleza visima vya Kimbiji na mradi wa usambazaji maji Kisarawe hadi Pugu (Gongolamboto, Pugu station, Airwing, Ukonga na Majohe).
Mingine ni; Mradi wa usambazaji maji katika mji wa Mkuranga na mwisho mradi wa bomba la kusafirisha maji kutoka Mlandizi- Chalinze hadi Mboga