Mbarali. Ibada ya kuaga miili minne ya familia moja ukiwamo wa bibi harusi mtarajiwa waliofariki dunia kwa ajali ya gari juzi alfariji eneo la Machimbo wilayani Mbarali mkoani Mbeya imefanyika na wamezikwa, huku bwana harusi mtarajiwa Elisante Edward akianguka wakati wa kumuaga mkewe mtarajiwa.
Bwana harusi Elisante ambaye ndiye alikuwa afunge ndoa na Diana kesho, alionekana kukosa nguvu za kuhimili kushiriki shughuli kutokana na uchungu wa kuondokewa na mke mtarajiwa.
Wakati anaaga miili hiyo, Elisante ameonekana kuishiwa nguvu na kudondoka chini kabla ya kusaidiwa na vijana wawili waliokuwa wakimshikiria muda wote baada ya kuiona sura ya mkewe mtarajiwa (Diana).
Ajali hiyo ilitokea juzi alfajiri barabara Kuu ya Mbeya-Makambako baada ya gari walilokuwa wakisafiria wanafamilia sita kutoka nyumbani kwao Chimala wilayani Mbarali kuelekea Dar es Salaam kugongwa kwa nyuma na lori aina Fuso na kusababisha vifo vya watu wanne na wawili kujeruhiwa. Gari hiyo baada ya kugongwa na Fuso ilitumbukia mtaroni na kupinduka.
Watu waliofariki dunia ni Diana Mwandunga ambaye alikuwa bibi harusi mtarajiwa, Faraja Mwandunga, James Mwandunga na mtoto wa Faraja, Jacton (2) wakati waliojeruhiwa ni Ibrahimu Mwandunga na Nico Mwandunga.
Familia hiyo ilikuwa inatoka nyumbani kwao Chimala kulikofanyika sherehe ya kumuaga bibi harusi ‘send off’ na ilikuwa ikisafiri kwenda Dar es Salam kwa ajili ya maandalizi ya 'send off' ya pili ya Diana iliyokuwa imepangwa kufanyika leo Ijumaa ya Juni 21. Send off ya kwanza ilifanyika Jumamosi iliyopita na harusi ilipangwa kufanyika kesho Jumamosi Jijini Dar es Salaam.