Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Apofuka kwa msongo wa kukosa mkopo

VIDEO: Apofuka kwa msongo wa kukosa mkopo

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama angeendelea na masomo yake Chuo Kikuu cha Elimu (Duce), Nelson Mubezi sasa angekuwa mwaka wa tatu akisubiri kumaliza masomo ya shahada ya kwanza ya ualimu.

Ndoto yake ilizima baada ya kukosa fedha kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na wakati akiwa katika harakati za kupata mkopo huo ili arejee chuoni, alipofuka macho na sasa Mubezi anajifunza maandishi ya nuktamkato katika kituo cha kusaidia walemavu cha Tanzania Bridge Centres for Disabled kilichoko Mbezi jijini hapa.

“Nateseka mno na mawazo, wadogo zangu na mama bado wananiangalia kwa kuwa baba yetu alifariki,” alisema Mubezi katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika kituoni hapo.

“Nimesomeshwa elimu ya sekondari kwa ufadhili tu. Bado nahitaji kufadhiliwa.”

Mubezi alilipiwa elimu ya sekondari, lakini hakupata mkopo kutokana na kusoma shule binafsi. Alipangiwa kuanza masomo Duce mwaka 2016 baada ya kufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza katika Shule ya Sekondari ya Katoke Lweru iliyopo mkoani Kagera.

Akijua kuwa hangeweza kulipiwa gharama za elimu ya juu na taasisi ya dini iliyosimamia masomo yake ya sekondari, Mubezi aliomba mkopo HELSB.

“Baba yangu alifariki na mama yangu yupo lakini ni mlemavu. Hivyo familia nzima iliweka matumaini kwangu,” alisema. “Nilihangaika sana kufuatilia mkopo na nilienda bodi mara tatu, lakini nilishindwa.”

Alisema chuo kilipofunguliwa, alienda kuanza masomo na wakati huo alijua muda wowote angepewa mkopo hivyo akaanza masomo.

“Nilimpigia simu mama nikaomba auze shamba tuliloachiwa urithi na baba ili nipate hela kidogo za kupanga chumba kwa sababu nilikosa hosteli. Mama aliuza akanitumia hela hivyo nikapanga Mtoni Mtongani,” alisema Mubezi.

Mubezi aliendelea kufuatilia mkopo HELSB mara kadhaa, lakini hakufanikiwa.

“Maisha yaliendelea kuwa magumu sana. Ikabidi niende kwa mlezi wa wanafunzi kumwambia tatizo langu. Hela kidogo aliyonitumia mama nayo iliisha kabisa kwa sababu ilishafika miezi mitatu,” alisema huku akibubujikwa na machozi.

“Baada ya kukwama kabisa nikalazimika kurudi Bukoba. Safari yangu ilikuwa ya shida sana. Nakumbuka sikula chakula kabisa. Niliwaza mengi; kwanza namna mama na wadogo zangu wanavyonitegemea, na pili jinsi ndoto yangu ya kusoma ilivyokwama.”

Alisema kwa kuwa tangu kidato cha kwanza mpaka cha sita alisoma kwa ufadhili wa shule ya Sekondari ya Katoke Lweru, alienda kuwataarifu kuwa hakupata mkopo na ameshindwa kuendelea na masomo.

Tatizo lake linajulikana kwa uongozi wa Duce, lakini si kwa undani alioueleza Mubezi.

Meneja wa kitengo cha habari, elimu na mawasiliano cha Duce, Dk Rodrick Ndomba alisema anafahamu kuwa Mubezi alifika chuoni, lakini hakusajiliwa kwa sababu hakulipa ada.

Lakini Mubezi alipata faraja na matumaini aliporejea shule aliyopata elimu ya sekondari.

“Walimu walinipokea na wakaahidi kunisaidia mwaka uliofuata kama ningerejea chuo,” alisema.

“Nilichanganyikiwa sana, nilikuwa na msongo mkubwa wa mawazo na wakati wote kichwa kilikuwa kinauma. Niliumia mno kuwa nyumbani wakati wenzangu wanasoma.”

Alisema wakati muda aliokuwa ameahidiwa kuwa angepata ufadhili ulipofika, kiongozi wa shule aliyoitegemea alihamishwa, taarifa ambayo ilimchanganya zaidi.

“Nakumbuka ilikuwa tarehe 25 mwezi wa nane mwaka juzi kipindi nilichodhani ningerudi shule niliamka asubuhi nikashangaa kuwa sioni,” anasema akikumbuka siku aliyopoteza uwezo wa kuona.

“Nilijua naota, nilihangaika huku na huko na kila nikifungua macho sikuwa naona chochote.”

Hapo ndipo alipoanza kushughulikia tatizo la macho, lakini wakati akihangaika kutibu macho walimu walimpa Sh2 milioni ili arudi chuoni, lakini walishachelewa; hakuwa anaweza tena kuona.

Badala yake kwenda shule, alitumia fedha hizo kutibu macho, lakini hadi leo hajafanikiwa.

Siku moja, anaeleza, alipata taarifa kuwa kuna kampuni jijini Dar es Salaam ambayo huwa inatoa msaada kwa walemavu wa macho kujifunza nukta nundu na akaamua kusafiri kuifuata.

Katika kutafuta, ndipo akapata kituo hicho cha Tanzania Bridge for Disabled cha Mbezi, ambacho kimempa matumaini mapya kutokana na kufundishwa elimu ya maisha na namna ya kukubali tatizo la kutoona.

Huku akisoma maandishi ya nuktanudu, Mubezi amefufua ndoto yake ya elimu; anatamani kurudi Chuo Kikuu kuendelea na masomo yake na anatamani Serikali imsaidie zaidi aweze kutumia maandishi hayo ili afikie ndoto yake.

“Nateseka mno na mawazo,” alisema.

“Huenda kilichosababisha nikose mkopo ni shule za binafsi nilizosoma. Lakini sikupewa nafasi kujieleza namna nilivyosoma.”

Hata katibu wa kituo hicho, Diana Mapunda ambaye pia haoni, anaamini kuwa Mubezi anaweza kuendelea na masomo ya elimu ya juu bila ya matatizo baada ya kufuzu maandishi hayo ya nuktanundu.

“Kwa sasa anajifunza nukta nundu na anaweza kuendelea na masomo ikiwa Serikali itampatia mkopo,” alisema Mapunda.

“Hiki kituo nilikianzisha baada ya kuona kuna watu wanapata ulemavu wa macho ukubwani lakini hawana msaada,” alisema.

Alisema alipewa namba ya usajili 2016-04-0536 na kwamba alitakiwa kulipa kiasi kidogo cha fedha kisha aahirishe masomo mpaka mwaka ujao, kama alikuwa na matatizo.



Chanzo: mwananchi.co.tz