Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VETA inavyomfanya Magufuli kukubalika Nkasi, Ileje

Cf8819113e20e0796e897092818c0cf1 VETA inavyomfanya Magufuli kukubalika Nkasi, Ileje

Thu, 27 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MIONGONI mwa mambo ambayo hayatasahaulika yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa wakazi wa wilaya za Nkasi mkoani Rukwa na Ileje mkoani Songwe ni watoto wao kuanza kupata mafunzo ya ufundi stadi katika wilaya zao.

Hii ni baada ya serikali kutimiza ahadi ya kujenga vyuo vya ufundi stadi (VETA) katika wilaya hizi mbili kama ilivyofanya pia kwa baadhi ya wilaya nyingine nchini.

Hizi ni wilaya zilizosahaulika kwa miaka mingi katika kupewa miradi mbalimbali ya maendeleo hususani inayolenga kuwapa ujuzi wakazi wa maeneo husika.

Julai mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alifungua matawi ya Veta katika wilaya hizi mbili. Mapokezi ya wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi waliobahatika kuwa wa kwanza kuanza kupata utaalamu kupitia vyuo hivi yalidhihirisha fika kuwa walikuwa wakisubiri huduma hii kwa shauku kubwa. Wazazi nao hawakubaki nyuma kuonesha furaha zao.

Akiwa katika tawi la Veta Palamawe lililopo katika kata ya Palamawe wilayani Nkasi, Ndalichako alisisitiza nia ya serikali kuendelea kuzalisha wahitimu wengi wa mafunzo ya ufundi stadi ili kuwezesha sekta hiyo kuwa na mchango katika uchumi na kuinyanyua Tanzania katika daraja la chini la uchumi wa kati iliyopo sasa kwenda madaraja ya juu.

Anasema mpango wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi utakuwa endelevu na kwamba lengo ni kila halmashauri kuwa na chuo cha Veta nchini ifikapo mwaka 2025 ili kuzalisha rasilimali watu wenye ujuzi na uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri.

Profesa Ndalichako anasema wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi wanachangia kwa kiasi kikubwa azma ya serikali ya kujenga nchi inayojielekeza katika uchumi wa viwanda.

Hata hivyo, anasisitiza kila Veta kujikita zaidi kwenye mafunzo ya ujuzi unaoendana na mazingira ya sehemu husika ili kuwezesha wahitimu kujiajiri mara tu wanapohitimu kwa kufanya shughuli kulingana na mazingira yanayowazunguka ili jamii zao pia zinufaike na mafunzo yao.

“Hapa Nkasi, kwa mfano, kuna wafugaji wengi na ngozi zimekuwa zikitupwa. Sasa leo hii tumeona katika kipindi cha muda mfupi wanafunzi chuoni hapa wameanza kutengeneza bidhaa za ngozi ikiwemo mkoba huu nilionunua kwa Sh 35,000. Ni hatua kubwa.

“Lengo la serikali ni kutoa mafunzo kulingana na mazingira ili ujuzi wanaopata vijana wetu wautumie walipo kwa kufanya kazi. Isiwe mara baada ya kuhitimu wanakutana na mazingira yasiyo rafiki. Kwa hapa ninasisitiza kitengo cha bidhaa za ngozi kiongezewe fedha ili kipanuliwe, kiwe kiwanda kabisa na mimi nawaahidi kuwatafutia masoko ya bidhaa mtakazozalisha,”anasema Ndalichako.

Kuanzishwa kwa chuo hicho kulitokana na kuchukuliwa kwa majengo yaliyokuwa ya mkandarasi aliyejenga barabara ya lami kutoka mjini Sumbawanga kwenda Kibaoni mkoani Katavi. Baada ya Kandarasi kumalizika majengo yalibakia mikononi mwa wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Rukwa.

Mkurugenzi mkuu wa Veta nchini, Pancras Bujuru, anasema Veta ilikabidhiwa majengo 13 kutoka Tanroads baada ya serikali kuridhia. Serikali pia ilitoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo na pia ununuzi wa samani za chuo.

Mabweni yaliyopo yana uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kwa wakati mmoja, wanawake 40 wanaume 40. Lakini kwa sasa uwezo wa chuo ni kupokea wanafunzi 120.

Tayari wanafunzi 43 wamehitimu katika chuo hicho tangu kilipoanza kutoa mafunzo mwaka huu na wengi wao wamejiajiri. Waliopo chuoni kwa sasa ni wanafunzi 35, kati yao wanawake ni 12. Kozi zinazotolewa kwa sasa ni ufundi umeme wa majumbani pamoja na ushonaji.

Aliyekuwa Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy ambaye amepitishwa tena na CCM kugombea nafasi hiyo anaomba wizara husika kukitazama kwa jicho la kipekee chuo hicho, kwani umuhimu wake ni mkubwa kwa vijana wa wilaya hiyo.

Mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mtanda anasema shauku ya kufunguliwa kwa chuo kwenye eneo lao ndiyo iliyosababisha wakazi wa kata ya Palamawe kujitoa kwa moyo pale waliposhirikishwa kufanya usafi wa eneo la chuo na pia kuikubalia serikali kutwaa moja kwa moja eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, anasema mkoa huo unahitaji vyuo vya mafunzo zaidi ili vijana waweze kupata ujuzi na kutoa mchango wao kwa taifa kupitia ajira au kujiajiri.

Wanafunzi Joseph Maneno, Renatha Bazil na Gaspar Mwaipopo wanaishukuru serikali kwa kuwapelekea chuo hicho na hivyo kuwawezesha kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kwenda mikoa mingine kupata ujuzi na kwamba wazazi walio na uwezo mdogo kimapato wangeshindwa kuwapeleka vijana wao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Palamawe, Paul Gwesa anasema chuo hicho ni mkombozi kwa watoto wa wakulima na wafugaji wilayani Nkasi. Wengi wao kipato chao ni cha chini hivyo walitamani watoto wao kuwa mafundi lakini wakashindwa kutokana na uwezo. Sasa chuo kimewafuata, jambo wanaloona ni hatua muhimu iliyofanywa na serikali.

Wakati hayo yakitokea wilayani Nkasi, wilayani Ileje nako mambo hayakuwa tofauti. Nderemo na vifijo vilitawala baada ya kuwasili kwa Profesa Ndalichako aliyewathibitishia kuwa mafunzo yanayotolewa na Veta Ileje ndiyo yanayotolewa kote nchini.

Veta ya wilaya ya Ileje awali ujenzi wake ulianzishwa na halmashauri ya wilaya hiyo kwa kujenga vyumba viwili vya madarasa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Mei 31, mwaka 2018 majengo hayo yalikabidhiwa kwa Veta ili iyaendeleze na kisha serikali ikatoa pesa ili kujenga chuo hicho.

Chuo hicho kina mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kila mmoja na nyumba ya mlezi wao, nyumba ya mkuu wa chuo na walimu. Chuo hiki kwa sasa kina fani tatu ikiwemo ya umeme wa majumbani na ushonaji nguo. Kwa kuanzia kina uwezo wa kupokea wanafunzi 60.

Aliyekuwa Mbunge wa Ileje, Janeth Mbene anashukuriwa pia kwa mchango wake katika kuhamasisha ujenzi wake.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nicodemus Mwangela anasema vyuo vya Veta ni muhimu kutokana na ongezeko kubwa la vijana wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za shule na kubaki mitaani.

Hata hivyo, licha ya bashasha zilizooneshwa na wakazi katika wilaya hizi mbili zilizoashiria kufurahia ujio wa Veta jirani na makazi yao, bado mwamko wa wazazi kuwapeleka watoto wao kujiunga na masomo kwenye vyuo hivi ni mdogo.

Hali hii ilimfanya Profesa Ndalichalo kusema endapo wakazi wa maeneo hayo watasuasua kupeleka watoto kupata stadi mbalimbali za ufundi, watafungua milango kwa vijana kutoka maeneo mengine nchini kwenda kunufaika na vyuo hivyo na kuwaacha wenyeji wakivitazama kama mapambo.

“Vyuo vya Veta ni vya Watanzania wote lakini tunajenga katika kila halmashauri ili wanufaika wa kwanza wawe vijana wanaopatikana kwenye eneo husika kabla ya wale wa mbali kuja. Sasa nawapa miezi mitatu iwapo mtaendelea kutotaka kutumia fursa hii hatutosita kuchukua mamuzi mengine. Uzuri hapa yapo mabweni tutachukua wanafunzi wa kutoka maeneo mengine waje kunufaika,”anasema.

Waziri anawataka wakazi wa wilaya zote kunakojengwa vyuo vya Veta kutambua kwamba nia ya Serikali ni kupanua wigo wa vijana nchini kuwa sehemu ya kushiriki jitihada za Serikali za kuimarisha uchumi na ndiyo sababu inatumia fedha nyingi kujenga vyuo vipya na kukarabati vya awali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Veta, Peter Maduki anazitaka halmashauri za wilaya zenye Veta sambamba na mikoa husika kuboresha mafunzo kwenye vyuo hivyo kwa kupeleka zabuni za kazi mbalimbali badala ya kupeleka kwa mafundi wa mitaani wasio na mafunzo.

Chanzo: habarileo.co.tz