Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzito na umaarufu wa jani la sale kwa Wachaga

32559 Jani+pic Tanzania Web Photo

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jani la sale ambalo ni la kimila katika Kabila la Wachaga linadaiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha kufikiwa kwa haki za wanawake na watoto wanaokumbana na vitendo vya ukatili ndani ya jamii hiyo.

Mbali na kuathiri haki, pia jani hilo linadaiwa kukwamisha kesi mbalimbali za ukatili zinazofikishwa kwenye vituo vya sheria kutokana na wahusika kulitumia kuombana msamaha.

Jani hilo linatajwa kuwa kikwazo kikubwa hasa katika kesi za ulawiti na ubakaji wa watoto, ambapo mtuhumiwa kwa kutumia wazee wa heshima hulitumia kuombea msamaha.

Jani la sale na imani iliyopo

Akizungumzia juu ya jani hilo, Clement Kwayu (71), mkazi wa Machame wilayani Moshi anasema ni moja ya majani yanayoheshimika katika mila za Wachaga kwani hutumika kwa matumizi mbalimbali.

“Sale linatumika kuweka mipaka ambapo katika kila shamba la Mchaga ni lazima jani hilo liwepo, na watu wawili waliopakana katika shamba husika ndio wanaohusika kulipanda jani hilo (kwa pamoja) na watu wote wanaheshimu mpaka huo,” anasema.

Anasema kuwa sale hutumika kuwapatanisha watu walio katika mgogoro na endapo mmoja atakosea na kuomba msamaha kwa kutumia jani hilo hakuna sababu ya kutoukubali msamaha huo.

Theresia Malya (62), mzaliwa wa Kibosho anaeleza kuwa jani hilo limekuwa likiheshimiwa na wazee na linatumika katika mila za Wachaga tangu enzi za mababu.

Anasema jani hilo pia linatumika kuwakaribisha wageni nyumbani. “Viongozi wa dini na Serikali wanapokwenda kutembelea maeneo mbalimbali katika ardhi ya Wachaga ni lazima wapokewe na (jani la) sale (ikiwa ni) ishara ya kuwepo kwa amani,” anasema.

Watetezi haki za binadamu

Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Ajiso, Virginia Silayo anasema jani hilo linakwamisha utendaji katika vyombo vya kisheria.

“Wapo watoto na wanawake wanaofanyiwa vitendo vya kikatili kama ulawiti na ubakaji, lakini wanashindwa kupata haki kutokana na wahusika kuombana msamaha kwa kutumia (jani la) sale,” anasema.

Ofisa Sheria wa Tume ya Haki za Binadamu Kanda ya Kaskazini, Frederick Lyimo anasema utu hauwezi kupewa thamani kwa kutumia jani na kwamba, matumizi hayo yanakiuka haki za binadamu kwa kiasi kikubwa. “Kamwe utu au thamani ya mtu haiwezi kulinganishwa na jani, ifike mahali jamii ibadilike ili watu waweze kufuata sheria,” anasema Lyimo.

Takukuru, wadau walia na sale

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, Hole Makungu anasema jani hilo halitafsiriwi kama rushwa kwani linaathiri pia utendaji katika kupambana na rushwa.

“Sale hatuwezi kuitafsiri kama rushwa kwani linaathiri upelelezi wa baadhi ya mashauri yanayohusiana na rushwa, wahusika wanakwenda kuombana msamaha na hatimaye tunakosa ushahidi,” anasema.

Ofisa wa Polisi Kitengo cha Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, ASP Zuhura Suleman anasema matumizi ya jani hilo la kimila yanawaumiza waathirika wa matukio ya ukatili.

“Wakati mwingine vitendo hivi vya kikatili vinafanywa na watu wa karibu kama mume kumpiga mke, watoto kubakwa au kulawitiwa na baba mzazi, baba mkubwa au mdogo na wajomba,” anasema.

Mchungaji Anna Makyao anaeleza kuwa sale ni jani la kimila na haliingiliani na imani yoyote na viongozi wa dini nao pia wanaliheshimu.

Hata hivyo, Padri Didas Ndetembea anasema jani hilo ni kikwazo katika kufikia uamuzi unaogusa haki za binadamu akisisitiza kuwa linasababisha baadhi ya mashauri kutomalizika ipasavyo mahakamani.

Chanzo: mwananchi.co.tz