Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uvunaji misitu kiteknolojia na  mchango wake pato la taifa

F21ada204544571ca9cf2a782b456baa Uvunaji misitu kiteknolojia na  mchango wake pato la taifa

Thu, 22 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SEKTA ya Maliasili na Utalii nchini inashika nafasi ya pili kwenye kuchangia pato la taifa ikiongozwa na kilimo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro, mchango wa sekta hiyo kwenye kwa pato la taifa ni asilimia 21 lakini mikakati uliopo ni kuongezeza zaidi makusanyo ili iwe ya kwanza.

Anasema utalii unachangia asilimia 17.3 na misitu asilimia 3.5, hivyo jitihada za wizara yake ni kuhakikisha misitu nayo inaongeza mchango wake hadi kufikia asilimia 10.

Dk Ndumbaro anasema misitu itachochea ongezeko la mapato iwapo sheria, sera na kanuni za uvunaji zitafuata misingi ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.

Anasema sekta hiyo inahitaji uwekezaji ambao utafanya misitu kuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Waziri anasema serikali katika kufanikisha hilo inatumia Sera ya Misitu ya mwaka 1998, Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 69, kifungu F ili kwa pamoja visikume usimamizi shirikishi na mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu kama ajenda kuu.

"Sisi tunaamini kuwa ushirikishwaji wananchi kwenye usimamizi na uhifadhi wa misitu ni mbinu muhimu kuifanya nchi ifikie uchumi wa kati wa juu kupitia rasilimali misitu," anasema.

Anasema Programu ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) inayotekelezwa kupitia Idara ya Misitu na Nyuki imeonesha ushahidi kuwa tenkolojia ni mbinu sahihi ya kuongeza mapato na undelevu wa misitu.

Waziri huyo anasema serikali za Tanzania na Finland zinafadhili programu hiyo huku matarajio yakiwa ni kuona matokeo chanya zaidi kwa siku zijazo.

Anasema ilani ya CCM Ibara ya 69 kifungu F, inasema sekta ya misitu inapaswa kuwa na mchango katika uchumi wa nchi kwa kuzingatia teknolojia.

"Tanzania tuna hekta milioni 48.1 za misitu, hii ikiwa ni takribani asilimia 54 ya eneo lote la nchi, hivyo tunapaswa kuitumia kwa uendelevu ili iwe na faida kwa nchi yetu," anasema.

Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa FORVAC, Juhan Harkonen, anasema mnyororo wa thamani utaonekana iwapo matumizi ya teknolojia katika uvunaji yatapewa kipaumbele.

Mshauri huyo anasema Finland wanatumia teknolojia katika uvunaji wa rasilimali misitu kwa wingi, hali ambayo imechangia misitu kuwa endelevu na pato la taifa kuongezeka.

"Sisi tumewekeza kwenye teknolojia ya uvunaji kwa kutumia mashine za kuchakata mazao ya misitu (na kuyaongezea thamani), hivyo kupitia FORVAC tutahakikisha hili linafanyika hapa nchini.

Tumenunua mashine hizo mbili, moja itatumika hapa Songea na Namtumbo na nyingine Ruangwa. Lakini hadi mwisho wa mwaka tunatarajia kununua mashine nyingine tatu,” anasema na kufafanua kwamba zitatumika katika kongani za Ruvuma, Lindi na Tanga.

Anafafanua kwamba mashine hizo zinazotumia dizeli kidogo, hupelekwa msituni na kisha kuzalisha mbao kwa ubora wa kimataifa na kwamba wakati mashine za zamani zilitoa mbao 10 kweye mtu mmoja, kwa mfano, mashine hizo huweza kutoa 15 au zaidi.

Anasema kwa ujumla mradi huo ambao unatekelezwa chini ya Idara ya Nyuki na Misitu ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland umeonesha mafanikio katika ngazi zote, jambo ambalo linawapa nguvu ya kuendelea.

Anasema Tanzania imejaaliwa eneo kubwa la misitu hivyo ikivunwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa itakuwa na tija kwa wananchi na nchi.

Mshauri huyo anasema teknolojia ya uvunaji mazao ya misitu itaweza kuisadia serikali kufuatilia na kujua aina ya miti ambayo inavunwa kwa mwaka na kiasi cha mapato ambacho kinaingia.

Anasema matumizi ya teknolojia yataongeza thamani ya mazao ya misitu hasa mbao kwa kuwa yatavunwa kwa ubora unaokubalika kwenye soko.

"Wakati mwingine bidhaa zinakosa soko kutokana na maandalizi hivyo tukitumia teknolojia thamani itaongezeka na upotevu wa mbao utakuwa mdogo," anasema.

Anasema kasi ya matumizi ya teknolojia inaendana na utafutaji wa masoko hivyo watahakikisha yote yanafanikiwa ili kuinua maisha ya Watanzania wanyonge wanaozungukwa na misitu.

"Changamoto ya soko inahitaji nguvu ya ziada kwani iwapo utawekeza kwenye teknolojia bila soko ni sawa na bure na hapo ndipo tafsiri sahihi ya mnyororo wa thamani itaonekana kwa kila mtu," anasema.

Harkonen anasema Tanzania ikitangaza bidhaa zinazopatikana kwenye misitu itapiga hatua kubwa kiuchumi hivyo watahakikisha hilo linafanikiwa.

Anasema Serikali ya Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo, mazingira na uchumi.

Mtaribu wa FORVAC Kitaifa, Emmanuel Msoffe mashine hizo zitachochea kupunguza upotevu wa hekta 469,000 kwa mwaka kutokana na kuvuna bila kufuata utaratibu.

Amesema iwapo teknolojia hiyo ya kutumia mashine za kisasa itasambaa nchini kote mazao ya misitu yataongezeka thamani na upotevu wa mbao kupungua kwa asilimia nyingi.

Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema mashine hiyo ya kisasa itasaidia kuondoa misumeno ya mnyororo maarufu (Chensoo).

Mutunda amesema mashine inayotembea itawezesha kupatikana kwa mbao nzuri ambazo hazitahitaji umaliziaji mkubwa kama zamani.

"Mbao ya mashine ya kisasa inayotembea ni bora kuliko hizi zilizochanwa kwa Chensoo tunaamini zikisambaa nchini kote bidhaa za mbao zitaongezeka thamani," amesema.

Naye Bwana Miti katika Kijiji cha Sautimoja wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, Yusuph Kiangio, amesema mashine ya kisasa ya kuchakata mbao inazalisha mbao nyingi kwa muda mchache na bora.

"Mbao tunazozalisha kwa mashine ya kisasa zinauzika kirahisi, lakini pia inaokoa upotevu wa mbao kwa asilimia 63 na matarajio yao ni kupata asilimia 80 ya mbao kwa gogo moja.

Ila pia asilimia 20 itakayobakia ambayo ni mabanzi, mbao fupifupi na unga ambao tunafikiria kuufanya mkaa," amesema.

Kiangio amesema katika wilaya Kilwa na Tunduru ambazo MCDI inafanya kazi wameweza kuongeza mapato kutoka shilingi milioni 26 kwa kuuza magogo lakini kupitia mashine hizo wamekusanya zaidi shilingi milioni 125.

Aidha amesema mashine hii inaweza kuzalisha mbao 250 kwa siku kutoka mbao 25 kwa siku.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Ezekiel Mwakalukwa anasema kinachofanywa na FORVAC, Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI) na wadau wengine katika kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu ndio hitaji la Serikali katika kumuinua mwananchi.

"Huu ni utekelezaji wa Sera ya Misitu ya 1998 na Sheria ya Misitu ya 2002 idara yangu na Serikali kwa ujumla tutaunga mkono kwa nguvu zote," anasema.

Anasema programu ya FORVAC itaweza kufikia lengo iwapo kila mdau atashiriki kwa kufuata sheria na miongozo inaliyoandaliwa na Idara ya Misitu na Nyuki kuhusu namna ya kutumia rasilimali hizo.

"Mashine hii ambayo inatolewa katika wilaya ya Songea na Namtumbo ni moja ya nyenzo muhimu kwenye kuonesha mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu ni matamanio yetu kuwa siku moja kila wenye uhitaji watapata," anasema.

Dk Mwakalukwa anasema idara hiyo itaendelea kutafuta wadau wa sekta hiyo ili kuhakikisha teknolojia inatumika kuongeza thamani mazao ya misitu.

Anasema jukumu lao kubwa ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii ambayo ina fursa ya rasilimali misitu ili iweze kutunza na kunufaika nayo kwa njia endelevu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Isabela Chilumba anasema mashine hiyo ni mkombozi mkubwa kwenye sekta ya misitu mkoani hapo.

Anasema imani yao ni kutumia mazao ya misitu kuinua uchumi wa wananchi, wilaya, mkoa na nchi kwa ujumla.

"FORVAC imekuja kutuletea mabadiliko makubwa kwenye sekta ya misitu ambapo sasa wananchi wanaanza kunufaika na rasilimali zao na kutokana na manufaa hayo, wanazilinda. Mashine hii ya kuchakata mazao ya misitu itakuwa kichocheo kikubwa zaidi," anasema.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho anasema teknolojia hiyo umekuja wakati mwafaka kwa kuwa inagusa ilani ya chama hicho.

Chanzo: www.habarileo.co.tz