Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uvaaji helmet Ilala bado pasua kichwa

5176438d62cce6cdc116ae4f6de80076 Uvaaji helmet Ilala bado pasua kichwa

Fri, 2 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

IDADI kubwa ya watumiaji wa usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda katika wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wanatumia usafiri huo bila ya kuvaa kofia ngumu (helmet), hali ambayo inahatarisha usalama wao ajali ikitokea.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya sehemu mbalimbali za Ilala kwa siku tatu umeonesha kwamba kuna uzembe mkubwa wa watu kutovaa kofia unaofanywa na baadhi ya waendeshaji wa pikipiki pamoja na abiria wao.

Si jambo la kushangaza kila pikipiki unayokutana nayo Ilala kukuta kati ya abiria au dereva mmoja hajavalia helmet au wote.

Katika vituo vya kuegeshea bodaboda katika eneo la Tabata Bima, Chama na Senene asilimia kubwa ya waendesha bodaboda waliokutwa walikuwa hawana kofia ngumu kwa ajili ya abiria ukiondoa za kwao. Hali kama hiyo pia ilionekana katika kituo cha Tabata Relini.

Hata hivyo, eneo ambalo waendesha bodaboda walikuwa na kofia ngumu mbili ni Buguruni Malapa, Boma, Sokoni na Garage lakini wakati wa kuondoa bodaboda kituoni mwandishi alishuhudia abiria wengi walionekana wakiwa hawajavaa kofia ngumu.

Akizungumzia kuhusu uvaaji wa kofia ngumu, mwendesha bodaboda wa Buguruni Malapa, Hassan Ndona anasema anavyoona ni kwamba kwa sasa hakuna msisitizo mkubwa wa kuvaa kofia ngumu.

Anapoulizwa sababu ya kudhani msisitizo wa kuvaa kofia ngumu hakuna anasema ni kwa kuwa hawakamatwi na askari kwa kutozivaa kama siku za nyuma.

“Kiasi cha mwaka mmoja uliopita, tulikuwa tunakamatwa na dereva kama mtu hajavaa kofia ngumu, iwe dereva au abiria tofauti na sasa,” anasema na kukiri kwamba wengi wanafuata sheria kwa kuogopa kukamatwa na siyo kwa ajili ya kulinda usalama wao.

Mkuu wa Polisi katika Mkoa wa Kipolisin wa Ilala, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Debora Magiligimba, anabainisha kuwa uvaaji wa kofia ngumu ni lazima na siyo hiari na kuhimiza wananchi kutii sheria bila shuruti.

“Askari wanaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa uvaaji wa kofia ngumu. Hata hivyo, waendesha bodaboda na abiria wanapaswa kutambua kuwa ni lazima kuvaa helmet, hilo siyo suala la hiari na hii ni kwa usalama wao,” anasema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Henry Bantu anawataka waendesha bodaboda na abiria kutambua kuwa zinasaidia sana kupunguza ukubwa wa majeraha.

Anafafanua kwamba pikipiki ikipata ajali huku abiria na dereva wakiwa wamevaa kofia ngumu zilizo imara ni wazi kwamba kuna uwezekano mkubwa wa majeraha watakayopata kuwa machache ikilinganishwa na pale wanapikuwa hawajavaa.

“Hakuna ujanja katika uvaaji wa helmet kwa kuwa tofauti na ilivyo kwa sehemu nyingine za mwili kuwa zikipatwa hitilafu kubwa zinaweza kukatwa kama mguu au mkono lakini vipi kwa kichwa. Kinaweza kukatwa? Nadhani jibu ni hapana hivyo hapa kuna umuhimu wa kuvaa helmet ili kuzuia vifo,” anasema.

Takwimu kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, zinaonesha kuwa Mkoa wa Kipolisi Ilala kwa mwaka 2019 kulikuwa na ajali 489, vifo 40, majeruhi 421 lakini mwaka 2020 ajali zilikuwa 114, vifo vilikuwa 26, majeruhi 196. Hivyo kuna utofauti wa ajali 375, vifo 14, majeruhi 225 sawa na upungufu wa ajali kwa asilimia 77, vifo asilimia 35 na majeruhi 53.

Anande Mwanshuru, Mkazi wa Tabata Liwiti ambaye kwa sasa ni mjane aliyeachiwa watoto wawili wadogo, anasema kuwa mumewe alikuwa mwendesha bodaboda ambaye alikufa kutokana na ajali iliyohusisha bodaboda yake aliyokuwa akiendesha na gari aina ya Fuso.

Anasema kuwa mumewe hakuwa amevaa bodaboda wakati Fuso hilo lilivyosukuma bodaboda yake na kuitoa nje ya barabara na kisha akapata majeraha yaliyosababisha kulazwa Hospitali ya Mifgupa Moi kwa siku mbili kabla ya kufariki dunia.

Kilichobainika ni kwamba Ilala inahitaji elimu na msisitizo wa kisheria katika kukabiliana na ajali. Sheria ya Usalama Barabarani ya 1973 inaonesha kuwa na mapungufu kwa kuwa imemtaja mwendesha bodaboda tu kwamba ndiye anapaswa kuvaa helmet.

Chanzo: www.habarileo.co.tz