Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uuzaji wa vyungu unavyowanufaisha wanawake Iringa

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mufindi. Wanawake wanaotengeneza bidhaa za udongo kama vyungu, majiko sanifu na mapambo ya nyumbani katika kijiji cha Lungemba, Mafinga wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa nchini Tanzania wameelezea namna kazi hiyo inavyowaingizia kipato.

Katika mazungumzo yao na Mwananchi hivi karibuni, wanawake hao wamesema soko wanalotegemea zaidi ni abiria wa mabasi na wasafiri wengine wanaopita katika barabara inayotoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na nchi jirani ikiwamo Zambia.

Mwenyekiti wao,  Zena Nyongole alisema kutokana na faida wanayoipata waliamua kuunda kikundi cha kiuchumi ili kiwasaidie kuweka akiba na kukopeshana fedha.

“Tuna uhakika wa kuuza bidhaa zetu japo soko tunalotegemea ni wasafiri peke yao, tunatamani kupata soko kubwa zaidi lakini changamoto inayotutesa ni mtaji, tunahitaji mtaji wa uhakika,” alisema Nyongole.

Mmoja wa wanakikundi hicho, Zena Lumato alieleza kupitia kazi hiyo amefanikiwa kujenga nyumba bora  na kusomesha watoto wake.

Mbunge wa Mafinga (CCM), Cosato Chumi amesema Jumatatu wiki ijayo atafanya ziara kwenye eneo hilo ili kuzungumza na wanawake hao.

Pia Soma

Advertisement
Chumi alisema kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi wanawake hao waliwahi kupewa mkopo mara mbili na safari ya nchini China kujifunza ubunifu chini ya Shirika la Viwanda vidogo (Sido)

 “Mara zote nawashauri kuwa lazima wajiandikishe na kusajiliwa na halmashauri ya wilaya ndipo wanufaike na mikopo, kwa mfano kwa sasa tunasema badala ya kuwapa pesa wananunuliwa vifaa kulingana na uhitaji wao,” alisema Chumi.

Chanzo: mwananchi.co.tz