Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utulivu watawala Rondo kwa Membe

Rondo Pic Utulivu watawala Rondo kwa Membe

Mon, 15 May 2023 Chanzo: Mwananchi

Utulivu umetawala nyumbani kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyefariki dunia Mei, 12, 2023 jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Kairuki.

Makazi ya Membe yapo katika kijiji cha Rondo Kata ya Chiponda ambako nyumba yake imo ndani ya eneo lisilopungua ekari mbili.

Ndani ya eneo hilo lililozungukwa na ukuta wenye rangi ya njano na nyeupe kuna nyumba kubwa ya familia, pembeni yake kuna nyumba za wafanyakazi pamoja na ofisi ya Membe ambayo ndani kuna maktaba iliyosheheni vitabu na nyaraka mbalimbali.

Tofauti na misiba mingine ambayo majirani hujazana na vilio hutawala kwa Membe ukimya ndiyo umetawala huku ukichagizwa na nyimbo za dini zinazopigwa na kusikika kutoka spika zilizofungwa

Katika makazi hayo. Ndugu na majirani wamekuwa wakiingia na kutoka kulingana na shughuli zao na kadri muda unavyokwenda ndivyo idadi yao inavyoongezeka

Kastro Membe ni mdogo wa marehemu, ambaye ameiambia Mwananchi Digital kuwa makazi hayo yamekuwa tulivu kwa kuwa majirani wengi wanasubiri mwili wa marehemu ufike.

"Unajua mazingira ya hapa ni tofauti kidogo kwa kuwa hakuna idadi kubwa ya watu kama ilivyo nje ya eneo hili ambako kuna majirani zetu, eneo hili tangu miaka mingi lilikuwa linakaliwa na wamisionari, lakini najua watu watakuwa wengi zaidi mwili ukiwasili," amesema.

Saida Jamal, ambaye ni jirani na Membe anasema wanamkumbuka kiongozi huyo kwa namna alivyokuwa akiwasaidia vikundi vya kina mama na vijana.

Zakayo Paul anasema Rondo wamepata pigo kwa kuwa Membe si tu alikuwa kiongozi wao bali ndugu aliyekuwa akiwasaidia kwa hali na mali.

"Mwili ukifika hapa nyumbani hali itakuwa mbaya zaidi, watu wanaweza kuzimia watakapoliona sanduku lenye mwili wa mpendwa wao" amesema.

Membe alifariki dunia Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Kairuki alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kukabiliwa na tatizo la kupumua.

Membe anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya Kanisa Katoliki ambayo pia yanatumiwa na familia hiyo.

Chanzo: Mwananchi