Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utiririshaji wa maji taka  wakati wa mvua ni hatari

3f0eabde1033bf6aef351fc8889aa59b Utiririshaji wa maji taka  wakati wa mvua ni hatari

Fri, 21 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATU hutegemea mvua ili kufanikisha shughuli mbalimbali, ikiwamo za kilimo cha bustani ndogondogo, kilimo cha mazao na wengine wakivuna maji hayo kwa matumizi ya kila siku najumbani.

Kinachokuwa tofauti ni kwamba baadhi yao hutumia fursa ya mvua kutiririsha maji taka katika mitaro ya kupitishia maji ya mvua na kusababisha kero kubwa kwa wapita njia na wakazi wa maeneo ya jirani na kutishia usalama wa afya zao.

Utiririshaji huo wa maji taka hayo, sehemu kubwa yakitoka vyooni na makaro ya maji machafu hufanyika huku shughuli mbalimbali za kijamii zikiendelea ikiwemo uuzaji vyakula na vinywaji hivyo kuhatarisha afya za walaji.

Ni jambo la kawaida kukuta mama lishe wakiendelea na uuzaji wa vyakula, juisi, maji ya kunywa pembezoni mwa barabara huku maji taka yakiendelea kutiririka.

Ajabu ni kwamba pale mvua inaponyesha jiji la Dar es Salaam kwa muda mchache tu, kiwango cha maji kinachotiririka barabarani na vichochoroni ni kikubwa kiasi cha watu kujiuliza maji hayo yanatoka wapi.

Mwanasheria kutoka timu ya wanasheria watetezi wa mazingira kwa vitendo yaani (LEAT), Mary Kessy anasema kuwa hali hii ya kutiririsha maji taka ovyo, imekithiri katika makazi yaliyojengwa kiholela bila ya kuzingatia mipango miji, kusiko na mitaa, mifereji na miundombinu ya kupitisha maji hayo.

Hata magari ya kwenda kunyonya maji taka katika makazi yaliyokosa mpangilio huwa ni ngumu kiasi kwamba, wakazi wa maeneo haya hutafuta mbinu mbadala ya kuyaondoa maji hayo.

Mbinu hizo ni kama kufungulia chemba ya maji taka majumbani mwao kisha maji hayo kujichanganya na maji ya mvua na kuelekea katika maeneo tofauti.

Aidha, sababu inayopelekea watu kufungulia chemba za majitaka wakati wa mvua kwa mujibu wa uchunguzi ni kwamba mtandao wa maji taka umepita maeneo machache. Hii inawapelekea watu kutafuta mbinu mbadala wa kuyaondoa maji taka kwenye chemba zao kwa kuyafungulia hasa kipindi cha mvua.

Kutokuwepo kwa magari ya kutosha ya utoaji maji taka, kunachangia kwa kiasi kikubwa kutopatikana kwa huduma ya utoaji maji taka kwenye kaya ambazo hazina huduma za mitandao ya maji taka.

Uwezo wa kumudu gharama za utoaji maji taka majumbani hadi sehemu ya kuhifadhi maji taka nayo ni changamoto nyingine kubwa kiasi kwamba watu wanashindwa kumudu gharama na kuona mbinu mbadala ya kuyaondoa maji taka ni kuyafungulia wakati mvua inanyesha, kitu ambacho kinaathiri mazingira kwa kiasi kikubwa.

Mbaya zaidi ni kwamba, mabomba ya maji safi yanayosambazwa kwa kila nyumba kwa matumizi, ambayo kwa wakati huo yanakuwa yamepasuka hujichanganya na maji taka hayo na hivyo kuweka afya za watu katika hatari kubwa.

Matokeo yake ni magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu katika kipindi hiki cha mvua, kwani wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo humpata mtu anayekula au kunywa maji yenye kinyesi cha binadamu chenye vimelea vya kipindupindu.

Kwa wanaokunywa maji yasiyochemsha, kwa mujibu wa ushauri wa wataalamu, hujijengea mazingira ya kuhatarisha afya zao.

Maji yakichemshwa kwa kiwango kinachotakiwa huondoa hatari ya mtu kukumbwa na magonjwa ya tumbo na kuhara.

Pia utiririshaji wa maji taka yenye sumu mathalani yanayotokea viwandani huchafua maji ya mito, maziwa na bahari, na kuharibu mandhari na nyakati nyingine kusababisha vifo vya viumbe kama samaki na mimea ipatikanayo ndani ya vyanzo vya maji.

Mwansheria huyo anasema kuwa sheria zipo na zinaelekeza kuwa yule ambae anafanya uharibifu wa mazingira achukuliwe hatua na si kufumbiwa macho kwani madhara yake ni makubwa mno kwa afya ya mwanadamu na mazingira kwa ujumla.

Ni wakati wa kubadilika na kushirikiana kupambana na magonjwa yatokanayo na maji kwa kuacha kutiririsha majitaka katika barabara, mitaro na kwenye vyanzo vya maji kama visima.

Serikali itafute mbingu za kupunguza gharama kubwa za kunyonya maji taka majumbani ili wengi wamudu gharama hizo.

Aidha, wananchi wapambane kuboresha usafi wa mazingira nchini ili kupunguza kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kama vile kuhara, kuhara damu, na minyoo.

Kinachotakiwa ni kubadilisha tabia na kuzingatia suala la usafi kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuhakikisha kuwa afya za watu zinalindwa kwa kiwango cha hali ya juu.

Halmashauri zote zinapaswa kuhakikisha kuwa kiwango cha maji taka kinachozalishwa kwenye maeneo yao kinakusanywa, kinasafirishwa na kumwagwa eneo husika bila kuathiri mazingira yetu.

Tushirikiane kwa pamoja kuyalinda mazingira yetu kwani mazingira yakiwa safi na salama, maisha yetu yatakuwa bora pia.

Chanzo: www.habarileo.co.tz