Wakati jamii na Serikali wakianzisha juhudi mbalimbali kupambana na umaskini, vijana mkoani Kilimanjaro wanawarudisha nyuma wazazi wao kwa kuwatelekezea watoto wa kulea na kushindwa kufanya shughuli za kujiingizia kipato.
Asilimia kubwa ya wananchi waliotembelewa na jopo la wahariri katika wilaya tatu mkoani humo ni wazee wanaolazimika kutunza wajukuu zao, baada ya vijana wao kukimbilia mijini na wengi wao kutofanya lolote kusaidia matunzo ya watoto wao.
“Ninaishi na wajukuu tisa,” alisema Donata Lucas Temba mwenye umri wa miaka 53 anayeishi Kata ya Karanga, Moshi Mjini na kuongeza.
“Kuna mtoto wangu aliniachia kichanga cha miezi mitatu tu, alikuja kujifungua baada ya miezi mitatu akatoweka.”
Mama huyo ana watoto sita ambao baadhi wameshamaliza shule, lakini hawana ajira inayoweza kuwasaidia kuendesha maisha, hivyo kutokuwa na msaada kwa mzazi wao.
Licha ya kutokuwa na ajira ya kuaminika, vijana hao wamekuwa wakizalisha au kuzaa na baadaye kuwapeleka watoto kwa bibi yao.
Advertisement “Unajua tena mzazi ni mzazi. Cha msingi ni kuhakikisha wanaendelea kuishi. Kama wanakuletea watoto utafanyaje? Unawakubali na kuwatuza,” alisema.
Donata ni mmoja wa wazee kadhaa katika Manispaa ya Moshi waliotelekezewa wajukuu na watoto wao na hawatumiwi fedha zozote kwa ajili ya kusaidia malenzi.
Wazee hao wamo kwenye baadhi ya kaya zilizotambuliwa na mamlaka za kata na mitaa kama familia zenye umaskini mkubwa na kuingizwa katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
“Kwa Sh80,000 nnilinunua kuku na kuuza, nikaanza kufuga mbuzi na baadaye nguruwe,” alisema Donata. “Angalau sasa namudu maisha ingawa ruzuku imepungua hadi Sh51,00.
Naye Mwajabu Idd Some, mkazi wa Bomambuzi ambaye pia anaishi na wajukuu watano alioachiwa na watoto wake, anaendesha maisha kwa kukaanga samaki katika kibanda alichojenga baada ya kupata ruzuku ya kwanza ya TASAF ya Sh68,000.
“Hizi fedha ninazopata hapa ndizo ninazozitumia kwa mahitaji ya shule ya wajukuu, kuongeza mtaji wa biashara na mambo mengine. Angalau sasa ninakula milo mitatu,” alisema.
Mwajabu pia amelazimika kuishi na wajukuu baada ya vijana wake kumuachia watoto hao kutokana na kutokuwa na ajira ya kuaminika kuwawezesha kuendesha maisha.
Pamoja na ugumu wa maisha, Halima Kondokaya, 52, amemudu kuwasomesha wajukuu alioachia hadi elimu ya sekondari baada ya kutumia vizuri ruzuku ya Sh40,000 kuimarisha biashara yake ndogo ya samaki wa kukakaanga.
“Sasa napata Sh20,000 kila baada ya siku kumi kutoka kundi letu la vikoba ambalo niliingia baada ya kuanza kupata fedha za TASAF,” alisema Halima ambaye ametengana na mumewe baada ya kutofautiana katika matumizi ya ruzuku hiyo.
“Watoto wangu walikuja kunitupia wajukuu hapa,” alisema Saidina Fred Kitalima anayeishi Mtaa wa Railway wakati akizungumza na wahariri kuhusu matumizi ya ruzuku anazopewa na TASAF), wiki iliyopita mjini Moshi.
Saidini, ambaye ni mke wa mfanyakazi wa Shirika la Reli (TRC) aliyepunguzwa kazini na sasa kaya yao ni wanufaika wa ruzuku za TASAF, amefanikiwa kusomesha watoto watano kati ya wanane, lakini sasa anaishi na wajukuu wanne.
Kundi la wahariri lililotembelea wilaya nyingine mbili za mkoani Kilimanjaro pia lilikutana na tatizo hilo la utekelezaji watoto.
“Kuna mzazi ambaye alimtelekeza mtoto kichanga kwa bibi yake kwa kudanganya anakwenda dukani, kumbe ndio alikuwa anatoroka na hajaonekana tena,” alisema Selina Wilson wakati wa majumuisho ya ziara hiyo ya wahariri kwa kaya zilizonufaika na ruzuku za TASAF.
Hata hivyo, Jolenice Bahati Ngowi, 70, amefanikiwa kumsomesha hadi kumaliza elimu ya sekondari mmoja kati ya wajukuu watatu alioachiwa na watoto wake.
“Mtoto wa kiume sijui yuko wapi, wa kike ananisalimia tu,” alisema Jolenice ambaye anaishi kwa kutegemea ruzuku, lakini hasa mifugo kama kuku, bata na mbuzi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashid Gembe alisema hadi sasa hawajafanya utafiti kujua tatizo la utekelezaji watoto ni kubwa kiasi gani, ingawa alisema kiwango cha umaskini mkoani Kilimanjaro ni kidogo.
“Hali ya umaskini mkoani Kilimanjaro si kubwa kutokana na nature (asili) ya wakazi kuwa wachapakazi,” alisema Gembe ambaye ndio kwanza amehamishiwa wilaya hiyo.
Katika wilaya hiyo, kaya 1,227 zilitambuliwa kuwa na kiwango kikubwa cha umaskini na hivyo kuingizwa katika mpango wa ruzuku wa TASAF.
“Hata hivyo, jukumu la kulea watoto ni la mzazi, hivyo kutotekeleza jukumu hilo ni kosa. Jukumu la kumlea mzazi ni la mtoto. Wazazi wanaotelekeza watoto wanafanya kosa mara mbili.”alisema Gembe.
Alisema Serikali inachofanya ni kuhakikisha wanatenga asilimia 10 ya mapato ya manispaa kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Tunawaomba vijana waje wapate mikopo isiyo na masharti au yenye masharti nafuu,” alisema.
Alisema katika kutekeleza hilo, mwaka jana zaidi ya Sh600 milioni zilitolewa kwa ajili ya vikundi vya kinamama, vijana na walemavu.
“Kulikuwa na vikundi 31 vya wanawake, 11 vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu,” alisema.
“Lakini taarifa zinaonyesha vikundi vya wanawake ndivyo vinavyofanya marejesho ya mikopo. Kazi yetu ni kuwakumbusha kulipa na hatua ya mwisho kama vikundi havilipi ni kuwapeleka mahakamani wahusika.”alisema.