Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata wizi wa vifaa vya Nida Arumeru, DC atoa siku tatu

Utata wizi wa vifaa vya Nida Arumeru, DC atoa siku tatu

Tue, 7 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Utata umetawala wizi wa vifaa vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wilayani Arumeru huku mkuu wa wilaya hiyo akitoa siku tatu kwa walioiba kuvirejesha.

Vifaa vilivyoibiwa ni kamera mbili, kompyuta mpakato mbili, kompyuta ya mezani moja, Keyboard, stendi mbili za kamera za mezani, extention za umeme mbili na damalog moja, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh7 milioni. Vilihifadhiwa katika jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC.

Hata hivyo, imebainika kuwa wizi huo umefanyika bila mlango kuvunjwa na nje kulikuwa na walinzi, lakini pia, jirani ya ofisi hizo kuna benki mbili zinazolindwa na polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amewaagiza Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na wizi huo ambao pia amesema umetokea katika mazingira ya kutatanisha kwa sababu wezi hao hawajavunja ofisi.

“Wafanyakazi wameingia ofisini, ndipo wakabaini vifaa hivyo havipo,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Muro pia ametoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana na akawaonya wananchi Arumeru, kuacha kununua vifaa hivyo kama vitafikishwa katika maeneo yao. “Ukimuona mtu anauza vifaa kama hivi, tafadhali tupe taarifa, usinunue ukifanya hivyo ni sawa na kununua nyara za Serikali,” alisema.

Alisema anatoa siku tatu kwa walioiba vitu hivyo, kuvirejesha wenyewe kabla ya kuanza msako mkali katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Hata hivyo, Muro alisema ameshangazwa na wizi huo, kwani ni mara ya pili kutokea wizi wa vitu vya Nida, hivi karibuni vifaa vingine viliibiwa.

Alisema katika tukio hilo watu wawili ambao ni mlinzi na mhudumu wa ofisi wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi.

“Wapo wafanyakazi wengine nao itabidi wahojiwe. Haiwezekani wizi utokee mara mbili katika ofisi hii na katika mazingira ya kutatanisha,” alisema Muro.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Nida wilayani Arumeru, Neema Nkya alisema aligundua wizi huo jana asubuhi baada ya kufika ofisini na kukuta vifaa hivyo vimeibwa.

Alisema kwamba hakuna mlango uliovunjwa na alimkuta muhudumu wa ofisi akiendelea na majukumu yake.

Nkya alisema kuibiwa kwa vifaa hivyo kutaathiri kazi ya utoaji vitambulisho vya uraia katika wilaya hiyo kutokana na kupotea kwa kumbukumbu muhimu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana alisema jana kuwa uchunguzi wa tukio hilo umeanza na akatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za wizi huo kuzipeleka polisi.

“Ni kweli tukio limetokea, lakini hakuna mlango uliovunjwa, sasa tunachunguza nini kimetokea na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika ambao watabainika,” alisema.

Kuibiwa kwa vifaa hivyo, kumekuja wakati wakazi wengi wa wilaya ya Arumeru waliojiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa tangu Agosti mwaka jana bado hawajapata.

Mkazi wa eneo hilo, Noah Lembrise alisema ni muhimu kwa vyombo vya dola kuchunguza tukio hilo, kwa sababu inawezekana kuna hujuma ndani ya ofisi za Nida ili kukwamisha kazi ya utoaji wa vitambulisho.

“Mimi nimejiandikisha tangu Agosti ingawa nimepata namba, lakini sijapata kitambulisho sasa kwa wizi huu, sijui hatma yangu kama kumbukumbu zangu zitapatikana,” alisema.

Usajili laini za simu

Katika hatua nyingine, mamia ya wakazi wa Arusha jana walijitokeza Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kusajili laini za simu na kupata namba za vitambulisho vya uraia.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliongoza kazi hiyo huku akitoa wito kwa halmashauri zote mkoani humo kutoa ushirikiano kwa Nida ili kuwezesha wananchi wote waliojiandikisha wapate namba za vitambulisho kwa wakati.

Wakizungumzia kazi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Zelothe Stephen na Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaban Juma wametoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha ili kusajili simu zao kabla ya Januari 20 siku ambayo laini zote zitakazokuwa hazijasajiliwa, zitazimwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz