Dodoma/Singida. Huku mamlaka ikithibitisha kuwepo mauaji ya kikatili, kuna utata wa idadi ya waliouawa wilayani Manyoni kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja.
Katika msiba wa katibu wa Chadema wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Alex Joas juzi, viongozi wa chama chake na wa CCM waliungana kupaza sauti kulaani mauaji hayo, wakisema vitendo hivyo vimekithiri na hakuna hatua zinazochukuliwa kuvikomesha.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbles Lema alidai katika mazishi hayo kuwa jumla ya watu 14 wamepoteza maisha katika wilaya hiyo kwa matukio ya mauaji yanayofanana katika miezi ya karibuni.
Idadi ya Lema ni tofauti na ya mbunge wa Manyoni (CCM), Daniel Mtuka aliyedai kuwa watu saba waliuawa kati ya Agosti mwaka jana na Februari, mwaka huu.
Mkuu wa wilaya hiyo alikiri kutokea mauaji na kuahidi kuyazungumzia kwa undani zaidi akiwa ofisini kuanzia leo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida naye aliahidi kulitolea taarifa suala hilo leo.
Habari zinazohusiana na hii
- Polisi yasema aliyeuawa Singida hakuwa kiongozi wa Chadema
- Baba wa katibu wa Chadema aliyeuawa Singida amuachia Mungu yaliyotokea
- Mwenyekiti CCM alaani mauaji kiongozi wa Chadema
- Mwili kiongozi Chadema aliyeuawa wawasili nyumbani
Lema, ambaye ni waziri kivuli wa mambo ya ndani, alissoma orodha ya watu aliosema wamekufa kwa kuchinjwa na kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani kumtimua kamanda wa polisi wa Singida na mkuu wa polisi wa Manyoni.
“Kwa orodha hii hapa si siasa. Naomba ndugu zangu makamanda wa Chadema msilipize kisasi. Hapa muungane ili kumpata mhusika anayewagombanisha, lakini msiwe wanyonge,” alisema Lema.
Kwa mujibu wa Lema, kifo cha Alex hakikuwa tofauti na wengine walivyouawa kwa mapanga na visu lakini hakuna wanaoshikiliwa, jambo linaloonyesha udhaifu wa polisi.
Kauli ya Lema iliungwa mkono na mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Jumanne Mahanda aliyevitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za makusudi kwa kuwa wananchi wanakwisha, lakini hakutaja idadi ya waliouawa.
Idadi ya mbunge Manyoni
Mbunge wa Manyoni Mashariki alisema anachofahamu watu saba ndio wameuawa katika kipindi cha kuanzia Agosti 2019 hadi Februari.
Alisema mazingira ya mauaji yanayotokea yanafanana, lakini alivituhumu vyombo vya dola kwa kutotoa taarifa za kina.
“Naomba wabunge wenzangu mnisaidie kupaza sauti. Hapa hakuna siasa bali kuna kitu nyuma ya pazia,” alisema Mtuka.
“Kumbukeni hata mwenyekiti wa Halmashauri ya Manyoni alipoteza binti yake wa kike, walimkata mapanga na kumburuza mita 10, inauma.”
Mbunge huyo alitaja eneo ambalo mwili wa Alex ulikutwa kwamba imeshatokea zaidi ya mara mbili, wiki mbili kabla ya Alex kuuawa. Alisema kijana mwendesha bodaboda alikatwa mapanga lakini akafanikiwa kukimbia huku mkono ukining’inia.
Mwanasiasa huyo alimuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Siro kuingilia kama watu wa chini yake wameshindwa kazi.
Akizungumza kwa simu jana, mkuu wa wilaya, Rahabu Mwagisa alithibitisha kutokea mauaji wilayani kwake, lakini akasema atatoa takwimu sahihi akiwa ofisini.
“Sijui Lema alipata wapi hizo takwimu, lakini kwa kweli mauaji yapo katika mazingira ya kutatanisha, ikiwemo watu kukatwa na mapanga bila sababu, lakini kesho (leo) nitakuwa katika nafasi nzuri ya kueleza wangapi wamekufa na kama kuna wanaoshikiliwa,” alisema.
RPC Singida
Kamanda wa Polisi Singida, Sweetbert Njewike alisema atatoa taarifa leo za idadi ya vifo vya watu wa Manyoni, namna walivyokufa na waliokamatwa.
Hata hivyo kabla ya jana, Njewike alishaeleza mkakati wa polisi kukomesha mauaji hayo.