Yuko wapi mtoto wangu, hili ndio swali analojiuliza Agnes Ngonyani, akimtafuta mwanae Ibrahim Ngonyani (22) aliyekuwa mikononi mwa Polisi mjini Arusha akiwa na jeraha la risasi begani linalodaiwa alipigwa na polisi.
Agnes anadai taarifa alizopewa mwanae (pichani) alikutwa kwenye tukio la ujambazi usiku wa Januari 23, saa 8 usiku eneo la Club Afriko, Kimandolu na alipigwa risasi na polisi na akawa mikononi mwao.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo alipoulizwa na gazeti hili jana alikiri kukamatwa kwa Ibrahim na pia kupelekwa mahakamani, lakini mama wa mtuhumiwa anadai kwenda hadi mahakamani na hakukuta kesi inayomhusu.
“Alipewa (Ibrahim) dhamana na kuna uwezekano aliruka dhamana akiwa nje, basi akatoweka au kutoroka kwa mara ya pili,” alisema Kamanda Masejo.
Hata hivyo, Agnes anadai kupewa taarifa zinazomchanganya kuwa mwanae alifariki akiwa mahabusu huku mmoja wa maofisa akimweleza kuwa waliamua kumwachia huru kwa vile jeraha la risasi lilianza kuoza. Kulingana na maelezo ya mama mzazi ambaye ni mkazi wa Kimandolu, anadai alidokezwa Ibrahim alikamatwa Januari 28, maeneo ya Kijenge lakini taarifa za kukamatwa zilimfikia Februari 8.
Alichokisema mama mzazi
Akizungumza na gazeti hili, Agness alieleza kupokea taarifa za mwanae kupigwa risasi katika tukio la uhalifu, lakini alitoroka na baadae alikamatwa na polisi na kushikiliwa na sasa hajulikani yuko wapi.
“Nililetewa taarifa na kiongozi wa Sungusungu, Alphayo Philipo kwamba Ibrahim alikutwa kwenye tukio la ujambazi usiku wa Januari 23, saa 8 eneo la Club Afriko, Kimandolu na alipigwa risasi na polisi,” alidai.
Taarifa za awali zinaonyesha baada ya mtuhumiwa kupigwa risasi, alitoroka lakini alikamatwa na polisi siku tano baadaye katika tukio jingine la uhalifu eneo la Kijenge.
Hata hivyo, mama yake hakuamini taarifa hizo kwa kuwa Ibrahim aliondoka nyumbani tangu Desemba 2022 kuwa anakwenda Dar es Salaam kwa kaka yake ili amsaidie kutafuta kazi.
Kulingana na maelezo yake, Machi 9, aliletewa taarifa na baadhi ya majirani kuwa wamesikia mwanae amefariki akiwa kituo cha polisi cha Kati, zilimshtua mama huyo na kukimbilia kituoni kumtafuta mwanae.
“Pale kituoni nilikutanishwa na aliyekuwa mpelelezi wa kesi, alikiri Ibrahim alikamatwa katika tukio la uambazi na alishafikishwa Mahakama ya Mwanzo Maromboso,” alidai.
Mama Ngonyani alidai alipokwenda mahakamani kufuatilia suala hilo aliambiwa hakuna kesi kama hiyo.
Machi 10 alirudi tena kituo cha polisi na kukutanishwa na mkuu wa upelelezi wilaya ya Arusha Mjini, afande Gwakisa ambaye alimpa taarifa tofauti na ile ya awali aliyopewa na mpelelezi, afande Habibu.
“Gwakisa aliniambia waliamua kumuachia mtuhumiwa (Ibrahim) baada ya kuona anazidi kuoza mkono kutokana na jeraha la risasi, hivyo kumpa fursa ya kwenda kupata matibabu.”
Kwa mujibu wa Agnes, kadri alivyokuwa akifuatilia kupata ukweli, alidai alianza kutishiwa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kumficha mhalifu na kumuuguza kwa siri kinyume cha sheria za nchi.