Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata vifo vya watu watatu walioteketea moto Moshi

Moto Moshi Watatu.png Utata vifo vya watu watatu walioteketea moto Moshi

Wed, 1 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vijana watatu wakiwemo wawili wa familia moja wamefariki dunia kwa kuteketea kwa moto katika kata ya Kibosho Kirima, wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuungua moto usiku wa manane huku tukio hilo likiwa limegubikwa na utata.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 29, 2023 wakati vijana hao wakiwa wamelala kwenye chumba kimoja ambapo miili yao iliungua moto kiasi cha kushindwa kutambulika.

Hata hivyo tukio hilo ambalo limeacha simanzi kwa familia na jamii limegubikwa na utata baada ya vijana hao ambao walikuwa wamelala kwenye kitanda kimoja mabaki ya miili yao yalikutwa ikiwa imelala chali, kuonyesha hakuna aliyejigusa wakati tukio hili linatokea.

Waliofariki kwenye ajali hiyo ni Emmanuel Mushi na Steven Mushi ambao ni madereva bodaboda pamoja na Felisichisimo Shio ambaye ni kinyozi ambapo wote ni wakazi wa kijiji cha Kirima kati.

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa, Mkaguzi Hassan Juma amethibitisha kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia Oktoba 29, mwaka huu na kwamba wakati wanafika eneo la tukio watu hao walikuwa wameshateketea kwa moto.

"Tulikuta nyumba imeshaungua moto na vijana watatu walifia ndani wakiwa wamelala, mpaka sasa chanzo hakijafahamika kwa sababu kulikuwa hakuna viashiria vyovyote vya moto vilivyoonekana.

"Tunashindwa kuelewa ilikuwaje watu watatu wakafia ndani bila hata kusogea kwenye godoro na kufia hapohapo bila kujigusa wala kujitetea, uchunguzi unaendelea ili tuweze kubaini chanzo cha moto huo,"amesema Kamanda Juma.

Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kisare Makori amesema baada ya kutokea kwa tukio hilo vyombo vya ulinzi na usalama vikiweno Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi walifika katika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji na kukuta miili ya watu watatu ikiwa imeteketea kwa moto.

"Ni kweli tukio la moto limetokea eneo la Kibosho , jeshi la polisi na zimamoto walifika wakakuta miili ya watu watatu ambayo kutoka na kuungua haikuweza kutambulika kwa muda ule, vyombo vyetu vinaendela na uchunguzi,"

Mashuhuda wasimulia tukio hilo

Boniface Soka, ambaye ni jirani na eneo lilikotokea tukio hilo amesema usiku wa manane akiwa amelala alisikia sauti ya baba wa mmoja wa marehemu ambaye ana tatizo la afya ya akili ikumuita bila kueleza chochote, hivyo hakutoka nje kwa kuwa alifikiri anaita kama ilivyo kawaida yake kuongea mwenyewe usiku, lakini muda mfupi baadaye alisikia kishindo kama cha mlipuko wa bomu, jambo lililompa wasiwasi.

"Nikiwa nimelala muda wa saa tisa usiku nilisikia mlipuko nikatoka kuangalia dirishani ili kujua ni nini, sikuelewa lakini niliona moto ukiwaka kwenye nyumba ya jirani, ndipo nilipompigia jirani yangu mwingine simu kwamba kuna nini mbona moto unawaka kwa jirani ndio tukatoka na kupiga simu kwa viongozi lakini nyumba tayari ilikuwa imeshateteketea na kulikuwa hakuna cha kuweza kuokoa,"amesema Soka.

Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Kirima kati, Patric Chuwa amesema baada ya kupigiwa simu alifika eneo la tukio na kukuta vijana hao tayari wameshatetea kwa moto ambapo kwa muda huo tayari gari la zima moto lilikuwa limeshawasili eneo la tukio, lakini hawakuweza kuokoa chohote kwani moto ulikuwa umeshateketeza kila kitu.

Amesema miili ya vijana hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC na kutokana na miili hiyo kuungua vibaya taratibu za mazishi zinaendelea katika familia zao baada ya ndugu kuweza kuitofautisha miili hiyo.

"Hii miili ya hawa vijana kwa namna ambayo tuliikuta kwenye kile chumba, tuliingiwa na utata mkubwa kwa sababu hawakujigusa walivyokuwa wamelala, tuliwakuta walivyokuwa wamelala wako hivyohivyo lakini kwa namna nilivyoona huu moto utakuwa umewashwa,"amesema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo, Inyasi Mushi ameliomba Jeshi la Polisi kuchunguza tukio hilo kwa kina na kama kuna hujuma zozote ambazo zimefanyika wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria maana ni tukio linaloumiza.

"Hawa vijana waliofariki ni wadogo sana, lakini kinachoumiza zaidi hawakuweza kunyanyuka pale kitandani kujitetea hata mmoja, wote walikufa palepale kitandani kama walivyokuwa wamelala,"amesema Diwani Mushi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live