Unaweza kusema ni utata kuhusu vifo vya vijana wawili wanaodaiwa kuuawa Mtaa wa Majengo, Vingunguti Darajani jijini hapa, baada ya Jeshi la Polisi kutoa maelezo yanayotofautiana na madai ya ndugu.
Vijana hao waliotajwa kuwa ni Shomary Kacheuka ‘Shomy’ (22) na Bakari Ismail ‘Beka’ (21) wanadaiwa kuuawa Desemba 27, mwaka jana walipotaka kuwashambulia polisi na wao kutaka kujihami na shambulizi hilo.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuwa mmoja wa wahalifu aliyekuwa akitafutwa na jeshi hilo alikuwa akizurura mtaani hapo.
“Mmoja wa watuhumiwa anayefahamika kwa jina la ‘panya kwaiti’ alikuwa anatafutwa na polisi, wakasema ameonekana akirandaranda maeneo ya Vingunguti,” alieleza Muliro.
Alisema jeshi hilo lilifuatilia nyendo za watuhumiwa na ilipofika saa 2:30 usiku askari walikutana nao maeneo ya Vingunguti darajani wakiwa watuhumiwa sita na kuwaweka chini ya ulinzi. Hata hivyo, alieleza watuhumiwa hao walikaidi amri na kutoa mapanga wakitaka kuwashambulia polisi hao.
Alieleza kwa kuwa eneo hilo lilikuwa giza, askari kwa kuhofia usalama wao wa kushambuliwa, walijihami kwa silaha za moto.
Kamanda Muliro alisema miongoni mwa kundi hilo, watatu walitambuliwa kwa jina moja moja ambalo ni Shomary, Bakari na Paka Pori.
“Watuhumiwa walipelekwa Hospitali ya Amana na baadaye walipoteza maisha. Jalada lilifunguliwa juu ya tukio hilo katika kituo cha polisi Buguruni,” alisema Muliro.
Alisema maiti zilizotambuliwa na ndugu na wazazi ni ya Shomary na Bakari, lakini mtuhumiwa mmoja aliyekuwa sehemu ya kundi hilo na wengine watatu walikimbia.
Familia zafunguka
Wakati Kamanda Muliro akieleza hayo, shangazi wa marehemu Shomary ambaye hakutaka kutaja jina alisema taarifa za mtoto wao kuwa alikuwa panyarodi zimewashangaza.
Alieleza mtoto wake aliuawa na polisi nyumbani kwake alipokuwa akiegesha pikipiki yake na wala si mtaani kama alivyoeelza Kamanda Muliro.
“Huyo kijana wangu siwezi kakubali wala kukataa kuwa ana tabia ya uhalifu kwa sababu alikuwa na shughuli zake zinazompatia riziki kwa kuuza spea za magari,” alisema shangazi huyo.
Alieleza siku hiyo polisi walifika mtaani kwao na kumkamata, wakati wanabishana kijana akitaka aelezwe anakamatwa kwa kosa gani, ndipo polisi walipompiga risasi yeye na mwenzake Bakari aliyekuwa akiwahoji polisi wanamkamata Shomary kwa kosa gani.
Alidai Bakari si rafiki wa Shomary, bali ni jirani yao na tukio la kupigwa risasi lilimkuta baada ya kutaka kufahamu kinachoendelea.
Kwa mujibu wa shangazi huyo, baada ya tukio hilo polisi waliondoka na vijana hao kusikojulikana ndipo alipokwenda vituo vyote vya polisi kikiwemo cha Buguruni ambako waliambiwa hakuna taarifa za kufikishwa watu hao.
“Niliulizia katika kituo kidogo cha polisi Vingunguti nikaambiwa hawana mtu huyo, nikafika kituo cha Tabata na tukaenda kituo kikubwa cha Buguruni na mkuu wa kituo alisema hana taarifa kama kuna tukio lilifanyika,”alisema.
Pia alisema waliambiwa hakuna taarifa za tukio la kutumika silaha maeneo hayo, hivyo zilipigwa simu katika vituo vingine vikiwamo Sitakishari, Msimbazi na Kinondoni kuhakikisha kama kuna taarifa hizo.
Alisema walirudi nyumbani ili asubuhi waendelee kuwatafuta kwa kuamini inawezekana kutokana na kipigo walishindwa kuzungumza, hivyo walirudi Desemba 28, 2023 asubuhi ili kufuatilia mahabusu lakini hawakufanikiwa.
Mbali na vituo hivyo, alisema walikwenda hadi kituo kikuu cha polisi kati na majibu yalikuwa yanafanana na ndipo walipoamua kwenda kumtafuta hospitali ya Amana, nako waliambiwa hakuna watu hao.
Kutokana na majibu hayo, walirudi kituo cha polisi Buguruni kwa ajili ya kufungua jalada la kupotelewa na ndugu yao hivyo waliambiwa warudi baada ya saa 24.
Alisema waliporudi nyumbani wakiwa wanajadiliana ndipo walipoletewa taarifa na msamaria kuwa vijana hao wapo hospitali ya Amana na hali zao ni mbaya..
Mjumbe wa Mtaa wa Majengo, Rajabu Ukongoro alisema mmoja wa marehemu ambaye ni Bakari hajawahi kuwa na rekodi ya uhalifu na shughuli yake kubwa ilikuwa ni kuosha magari na pikipiki.