Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata uchunguzi majitope Mwadui

Majitakaaaaaaa Utata uchunguzi majitope Mwadui

Mon, 14 Nov 2022 Chanzo: mwanachidigital

Wadau na wabobezi kwenye sekta ya madini wameshauri iundwe timu huru ya uchunguzi kujiridhisha na athari ya majitope yanayotiririka kwenye vijiji baada ya bwawa la mgodi wa almasi wa Williamson Diamond Limited (WDL), kubomoka.

Kauli ya wabobezi hao imekuja wakati matokeo ya awali kuhusu majitope hayo yakionyesha kutokuwa na madhara kwa binadamu.

Bwawa hilo lilibomoka Novemba 7, mwaka huu na kuundwa kamati ya uchunguzi siku chache baadaye inayohusisha wataalamu kutoka Tume ya Madini Tanzania (TMC), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira (NEMC), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, bonde la maji na kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Shinyanga na kanda ya ziwa.

Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la NEMC, Dk Samuel Gwamaka aliwaambia wanahabari kuwa tope hilo lililosambaa kilomita nane sio topesumu, na hakuna madhara yaliyojitokeza katika matokeo ya vipimo vya awali vya uchunguzi uliofanyika nchini.

“Hatua za awali ni kusimamisha kabisa matumizi ya bwawa na uzalishaji, kwa sasa matokeo ya awali vipimo yameonyesha hali sio ile ya hatari tuliyokuwa tukiihofia,” alisema Gwamaka, wakati wa ukaguzi wa maeneo yaliyoathiriwa na maji hayo.

“Lakini lazima mgodi upigwe faini na wapime kwa ujumla wake wote, mbali na kuchafua mazingira, athari ni kubwa, kwani limegusa eneo la leseni na maeneo nje ya leseni,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Meneja Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa, Musa Kuzumila alisema wamefanya upimaji wa maji na tope ya bwawa hilo na kubaini hayana madhara kwa binadamu na wanyama, hivyo wananchi wanaruhusiwa kutumia na kunywesha mifugo kama kawaida.

Hata hivyo, Shirika la Usimamizi wa Viwango vya Kimataifa katika mabwawa ya topesumu (GISTM), linaelekeza uwepo wa bodi huru ya ukaguzi wa mabwawa (ITRB), katika hatua za uchunguzi wa aina hiyo ili kutathmini mambo yanayohusiana na uamuzi na uhandisi yaliyochagiza kubomoka kwa bwawa hilo.

Mgodi huo unazalisha madini ya almasi chini ya uendeshaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Uchimbaji Almasi ya Petra Diamond inayomiliki asilimia 63 ya hisa, huku Serikali ikimiliki asilimia 37.

Akilizungumzia hilo, Lindsay Bowker, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uchunguzi wa Mabwawa hayo la Marekani (WMTF), alisema bodi hiyo ni muhimu kujiridhisha kuhusu uamuzi unaotokana na mazingira ya kubomoka kwa bwawa hilo.

“Serikali na Petra walipaswa kuagiza ITRB baada ya kubomoka bwawa hilo, kwa sababu limeboka ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kampuni hiyo ya WDL kuongeza uwezo wake wa uzalishaji bila ya kuongeza uwezo wa bwawa lake, kwa hiyo ni muhimu ITRB kushirikishwa,” alisema Lindsay.

Uanzishwaji wa ITRB umejikita katika masuala mbalimbali yanayohusiana na uchunguzi wa mabwawa, muktadha wake na utata wa suala hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa mapitio huru ya kiufundi ya muundo, ujenzi, uendeshaji, kufungwa na usimamizi wa kituo.

Alisema hakuna juhudi za kupunguza majitope kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita katika bwawa hilo lililobomoka.

Kwa upande wa Mhandisi Peter Kaheshi, ambaye kwa sasa anasomea shahada ya udaktari inayohusiana na usimamizi wa taka za mabwawa ya migodi nchini Canada, alisema: “Hili ni jambo lisiloepukika, kampuni inahitaji kufanya usafi na kutathmini uwezo wa bwawa lake, pamoja na kutekeleza hatua za kiufundi zinazoonekana kuwa muhimu ili kuepuka matukio kama haya katika siku zijazo”.

Akizungumza baada ya matokeo ya awali ya tathmini hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema alisema awali wananchi walishindwa kutumia maji kwa kuhofia madhara, lakini vipimo vimewaondolea hofu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude alisema baada ya taarifa za wataalamu kuhusu usalama wa maji hayo, sasa wanaendelea kutumia na kunyweshea mifugo.

Chanzo: mwanachidigital