Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata kifo cha aliyekutwa na kanga shingoni

MAUAJIZ.png Utata kifo cha aliyekutwa na kanga shingoni

Thu, 6 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Utata umeibuka kuhusu kifo cha mkazi wa Tabata Segerea jijini Dar es Salaam, Piariz Hiza (31) ambaye mwili wake unadaiwa kukutwa sakafuni chumbani kwake ukiwa hauna nguo, huku ukiwa na kipande cha kanga shingoni na kingine kikining'inia kwenye feni.

Akizungumza mdogo wa marehemu, Focus Hiza alidai taarifa za kifo cha dada yake alizipata Jumapili akiwa safarini akitokea Lushoto mkoani Tanga kwenda Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu za kifo hicho.

"Tunachunguza tukio hili, tunamhoji mume wake, maana kushikiliwa ni jambo lingine na kukamatwa ni jambo lingine. Mtu akipoteza maisha huwa tunahoji kujua sababu ya kifo ni nini, ukisema amenyongwa halafu taarifa ya daktari zikakuta kitu kingine, tunachunguza.

"Au ni sawa sawa unikute nimekufa, nina jeraha shingoni halafu ukasema kwa vyovyote nimeuawa. Hakuna mtu anajikata kisu anakufa, ni kupeleleza. Hii ndiyo njia nzuri ya kutenda haki, jambo hili linachunguzwa," alisisitiza.

Akisimulia kuhusu tukio hilo, mdogo wa marehemu, Hiza, alidai kuwa akiwa kwenye basi, alipigiwa simu na ndugu yake aliyeko Lushoto, akimjulisha kuhusu kifo cha dada yake ambaye alikuwa akiishi Tabata Segerea eneo la Kwa Bibi na hatua ya kwanza aliyochukua ni kupiga simu kwa msaidizi wa kazi za ndani wa dada yake aliyedai anaitwa Janeth.

"Janeth alipopokea akawa analia, nikamuuliza 'Janeth kuna shida gani?', akasema, 'dada kajiua', nikamuuliza 'kajiuaje?', akaniambia 'shemeji ametoka ndani analia, anasema 'dada yenu amejinyonga'. Nikamuuliza Janeth kama  ameingia chumbani na kuuona mwili, akanijibu 'ndiyo, nimekuta dada amelala sakafuni' na alipofika nyumbani kwa dada yake, aliingia chumbani na kushuhudia alichokuwa amedokezwa.

"Niliwakuta askari polisi wameshafika nyumbani kwa shemeji lakini wakati ninafika walikuwa hawajaugusa (mwili), hawajafanya chochote.

"Nilimkuta dada kalala sakafuni, hana hata nguo, walikuwa hata hawajamfunika, tukamfunika, nimemkuta dada sehemu ya shingoni kuna kipande cha kanga kimefungwa na kingine kikiwa kinaning'inia kwenye feni," alidai.

Aliendelea kudai kuwa mwili wa dada yake aliuona ukiwa na majeraha ya kuviria damu maeneo ya kifuani na shingoni, akibainisha kuwa baada ya uchunguzi wa polisi nyumbani kwa dada yake, mwili ulichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live