Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata idadi ya vifo magari yaliyokuwa yakikimbizana

53646 Pic+utata

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha/Moshi. Utata umeibuka idadi ya vifo vilivyotokea juzi katika ajali iliyohusisha magari mawili yaliyokuwa yakikimbizana eneo la Oldonyosambu wilayani Arumeru, Arusha.

Utata huo umekuja baada ya kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Jonathan Shana kudai kuwa vifo vilivyotokea ni viwili, miongoni mwao yumo raia mmoja wa Kenya, lakini ofisa wa ubalozi huo aliyeomba jina lake lihifadhiwe kwa kuwa si msemaji, alidai Wakenya waliofariki dunia ni watatu.

Hata hivyo, Kamanda Shana alisema baadaye, “tumepata taarifa idadi imeongezeka, ndiyo tunafuatilia kwa sababu kulikuwa na majeruhi wengine ambao hali zilikuwa mbaya, idadi inaweza kuongezeka.”

Awali aliwataja waliofariki baada ya ajali hiyo kuwa ni Robin Njiru, raia wa Kenya na Peter Mushi, Mtanzania mkazi wa Kijenge mjini Arusha na watu watano walikuwa wamejeruhiwa.

Hata hivyo ofisa wa ubalozi alisema Wakenya waliofariki ni watatu na majeruhi mmoja aliyemtaja kwa jina la Stella Muthoni Mungai (21) ambaye amelazwa hospitali ya Selian.

Ofisa huyo aliwataja raia wengine wa Kenya waliofariki kuwa ni Linet Mutio Kamau na Onesmus Mwangi ambao walisafirishwa jana mchana na ndege ya kukodi kutokea uwanja mdogo wa Arusha.

Mwananchi lilishuhudia majeneza matatu yakipakiwa kwenye ndege.

Ajali hiyo iliyohusisha magari aina ya Toyota iliyosajiliwa Kenya na nyingine aina hiyo iliyosajiliwa Tanzania inadaiwa yaligongana wahusika walipokuwa wakishindana kwenda kula nyama choma eneo la Oldonyosambu ambalo mara nyingi hutumiwa na vijana wenye magari kwenda kupumzika baada ya mashindano hayo.

Wakati utata kuhusu idadi ya vifo ukiwa bado haujateguliwa, taarifa za kifo cha mpigapicha maarufu mjini Moshi, Eric Fabric Urassa anayedaiwa kufariki dunia katika tukio hilo zimetikisa mji humo.

Taarifa hizo za Eric, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), zilianza kusambaa kwa kasi juzi saa 12:30 jioni muda mfupi baada ya ajali hiyo. Inaelezwa kuwa aligongwa na magari hayo yaliyopata ajali na tangu juzi na jana, picha zake zinasambazwa zaidi katika mitandao ya kijamii na makundi ya WhatsApp zikiambatana na maneno ‘RIP Eric Fabric’ na ‘pumzika kwa amani ndugu yetu Eric’.

Taarifa kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na picha yake muda mfupi kabla ya ajali, zilidai Eric alikuwa kando ya barabara akitekeleza jukumu lake la upigaji picha.

Imeandikwa na Filbert Rweyemamu, Mussa Juma na Daniel Mjema



Chanzo: mwananchi.co.tz