Arusha. Jiji la Arusha limetangaza utaratibu wa kuteketeza mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi, 2019.
Akizungumza leo Jumanne Mei 28, 2019 ofisa afya na usafi wa mazingira wa Jiji la Arusha, James Lobikoki amesema wafanyabiashara wenye mifuko kuanzia kilo 500 na kuendelea wanapaswa kuipeleka dampo lililopo eneo la Murieti.
Lobikoki amesema wenye kilo chini ya 500 wanatakiwa kupeleka mifuko hiyo katika ofisi za serikali ngazi ya kata ili kukusanywa na kupelekwa dampo kuteketezwa.
"Tunaamini wenye akiba ya mifuko watatekeleza maagizo haya ili kutekeleza agizo la Serikali kupiga marufuku mifuko hiyo,” amesema.
Akizungumzia mifuko mbadala amesema tayari wajasiriamali kadhaa wameanza kutengeneza na akawaondoa hofu wakazi wa jiji juu ya kubeba bidhaa zao.