Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utambuzi wa visima Dar waanza

10448 VISIMA+PIC TanzaniaWeb

Sun, 1 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na uchimbaji wa visima kiholela bodi ya maji ya bonde la Wami Ruvu imeanza utambuzi wa visima katika Jiji la Dar es Salaam ili kukabiliana na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha watendaji wa kata zilizopo manispaa ya Temeke, ofisa maji wa bonde la Wami Ruvu, Simon Ngonyani amesema uchimbaji holela wa visima umeleta madhara kadhaa,  hivyo ni muhimu ukaguzi kufanyika kabla ya kisima kuchimbwa.

Amesema uchimbaji huo ukiendelea bila kufuatwa utaratibu upo uwezekano wa kukausha miamba inayohifadhi maji na kusababisha ardhi kutitia.

 “Kufuatia athari zote hizo tumeona tufanye utambuzi wa visima vyote, tujue viko wapi na vina hali gani tukiona kuna kisima hakiko sawa tutakifungia na kuanzia sasa mtu anayetaka kuchimba kisima lazima apate kibali,” amesema

“Hali ni mbaya sana katika jiji la Dar es Salaam kila unakopita unakutana na kisima watu wakiamini kwamba ndio suluhisho la maji, hilo halipingiki ila lazima kuwe na utaratibu usichimbe kisima bila kibali,”

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, mhandisi Primy Damas aliwataka watendaji wa kata kuhakikisha wanasimamia sheria kukabiliana na watu wanaovamia na kuharibu vyanzo vya maji.

Amesema kuna ulegevu wa usimaizi wa sheria jambo linalochangia vyanzo vya maji kuvamiwa na shughuli za kibinadamu.

Mtendaji wa kata ya Chamazi, Harrison Mrema amesema changamoto kubwa ipo kwa wananchi ambao baadhi yao licha ya kuelewa sheria na taratibu wanazivunja kwa makusudi.

Chanzo: mwananchi.co.tz