Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utakatishaji Fedha, CCM yatuhumu kina Mbatia

32934 Pic+mbatia Tanzania Web Photo

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Moshi Vijijini kimeitaka Serikali kuichunguza Taasisi ya Maendeleo Jimbo la Vunjo (VDF) kwa madai ya utakatishaji wa fedha.

Miongoni mwa viongozi wa bodi ya VDF ni Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia ambaye na mwenyekiti wake wamekanusha tuhuma hizo.

Katika taarifa iliyosainiwa na Katibu wa CCM wilaya hiyo, Miriam Kaaya chama hicho kimeitaka VDF ieleze ilianza na kiasi gani cha fedha na bajeti ya barabara inazojenga ni kiasi gani.

“Tunaitaka VDF itamke wazi kuzithibitishia mamlaka za Serikali ilianza na kiasi gani cha fedha katika akaunti yake na bajeti nzima ya mradi wa barabara za moramu kwa Jimbo la Vunjo”.

“VDF itamke ilitarajia wananchi wa Jimbo la Vunjo wachangie kiasi gani. Kwa kufanya hivyo itaondoa uwezekano mkubwa wa asasi hiyo kutumika katika vitendo vya utakatishaji fedha,” taarifa hiyo ilisema.

Chama hicho kimeitaka Serikali kusitisha shughuli za taasisi hiyo wakati uchunguzi ukiendelea.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa VDF ambaye ni Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao amesema hawajapokea fedha yoyote kutoka nje na kwamba fedha wanazotumia kutekeleza miradi zinatoka kwa wananchi.

Naye Mbatia ambaye ni katibu wa taasisi hiyo alisema yote yaliyosemwa na CCM ni uongo na ni watu wanaotapatapa na kwamba watachukua hatua za kisheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz