Shirika la Afya women Group kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali wamefanya utafiti wa stadi za maisha na maadili kwa vijana katika Wilaya ya Mufindi, wenye umri wa Miaka 13 hadi 17 huku Wilaya hiyo ikionyesha kufanya vizuri katika utafiti huo.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa wa utafiti huo wa Mradi wa - Alive Christina Swai wakati wa kutoa taarifa kuhusu uzinduzi wa utafiti wa tathimini ya stadi za maisha na maadili kwa Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa ambayo imefanyika katika Shule ya Msingi Upendo, Kata ya Upendo Halmashauri ya Mji Mafinga. Swai amesema kuwa katika utafiti huo umeonyesha kwamba asilimia kubwa ya vijana wenye umri huo katika Wilaya ya Mufindi wapo katika kiwango cha pili huku vijana 3 kati ya 10 ndio wanaweza kutambua kuwepo wa tatizo wakiwa na mtazamo mmoja na kuchukua hatua ya kutatua changamoto hiyo
Aidha ameeleza kuwa stadi za maisha na maadili ni hali ambayo inaweza kuwasaidia vijana katika ukuaji wao kwa ngazi mbalimbali ikiwemo ukuaji wa kiafya pamoja na kiakili. Amesema kuwa katika utafiti huo ulikuwa umelenga katika Makundi manne ambayo ni kujitambua, ushirikiano, utatuzi wa matatizo pamoja na heshima. Kwa upande wake Mratibu wa Afya Women Group Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Nyaki Gabriel amezitaja nchi za Afrika Mashariki ambazo zimeshiriki kwenye utafiti huo kuwa Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi pamoja na Sudani Kusini. Pia Mratibu huyo amefafanua kwamba utafiti huo imefanyika katika Wilaya 20 ambapo kwa Mkoa wa Iringa utafiti huo imefanyika katika Wilaya ya Mufindi pekee ambapo imeonyesha kufanya vizuri Kwenye utafiti huo. "Utafiti huo ulilenga kufanyika katika maeneo halmashauri zote ya Mji Mafinga pamoja na Halmashauri ya Wilaya Mufindi ili kuweza kutathimini stadi za maisha na maadili kwa vijana upo katika kiwango gani ili wazazi na walezi waweze kuwasaidia watoto wao." Amesema Gabriel.