Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushirika Dar watoa ushauri serikalini, watofautiana hesabu za fedha

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Ushirika wa Viwanda vidogo Dar es Salaam (Dasico) nchini Tanzania, kimeiomba Serikali kufanya ziara kutembelea chama hicho ili kutoa ushauri utakaowezesha kuboresha chama hicho.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 7,2019 katika mkutano wa mwaka kujadili mafanikio na changamoto ndani ya chama Mwenyekiti wa Dasico, Mfaume Yusuph amesema licha ya vyama hivyo kuwa vingi hapa nchini lakini vinasahaulika na havipewi kipaumbele.

Amesema ushauri kutoka serikalini ni muhimu kwani utasaidia kuongeza mbinu za kuboresha vyama hivyo ambavyo vipo zaidi ya 200 hapa nchini.

“Hivi vyama vipo muda mrefu lakini vinasahaulika sana, sisi tunaomba watutembelee wasisubiri kuja kutuchukua tu kipindi cha maonyesho na badala yake watutembelee waone changamoto zetu,” amesema Mwenyekiti huyo

Ameongeza kuwa majadiliano katika mkutano huo wenye wanachama 268 yatatoa mwanga wa namna ya kuboresha chama hicho lakini pia kuchangia maendeleo ya chama na uchumi wa nchi.

“Hali siyo nzuri kidogo kwa upande wetu katika ukaguzi wetu tumebaini hasara ya Sh8 bilioni hii ni kutokana na uchakavu wa miundo mbinu yetu lakini pia hata mtaji wetu umeshuka kutoka Sh3.7 bilioni mwaka jana hadi Sh3.6 bilioni mwaka huu.”

Pia Soma

Hata hivyo, amewaomba wanachama kushirikiana na idara kwani ushuru waliokusanya haukuweza kufikia malengo na kuongeza kuwa hali hiyo ni hatari kwa ustawi wa chama.

Wakati mjadala ukiendelea baadhi ya wanachama walitofautiana na uongozi wao na kutaka kujua hasara hiyo ya Sh8 milioni imetokana na nini.

Mmoja ya wanachama hao Hamisi Issa ametaka ufanyike uchunguzi wa kiofisi kubaini hasara hiyo lakini pia wanachama hawaajui matumizi ya fedha hizo.

“Sheria inaruhusu uchunguzi ili kila mwanachama ajue Sh8 bilioni ni nyingi sana yasifanyike mambo juu juu tu ufanyike uchunguzi wa kiofisi ipo haja Dasico kukaa na kupanga mwelekeo wa chama bila kufanya hivi hali itakuwa mbaya ipo haja ya kukuza uchumi wetu,” amesema mwanachama huyo.

Hata hivyo, mwenyekiti amewaomba wanachama hao kuwa wapole na kukiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuongeza kuwa watazipatia ufumbuzi, “hata sisi tunazijua changamoto hizi hapa tulipo hatuna  hata mashine za kisasa za kufanyia kazi tuvumiliane.”

Chanzo: mwananchi.co.tz