Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri wa mwendokasi waitesa Serikali

Wed, 5 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mradi wa mabasi yaendayo haraka wa jijini Dar es Salaam ukianza kulalamikiwa siku za hivi karibuni na wakazi wanaoishi maeneo ulikopita, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amewataka watumiaji wa usafiri huo kuwa watulivu kwani mambo mazuri yanakuja.

Kamwelwe ametoa kauli hiyo jana katika mkutano wa mwaka wa usafirishaji uliowakutanisha pia wadau wa maendeleo, mabalozi wa nchi mbalimbali na sekta binafsi.

Alisema changamoto zinazoonekana sasa kwenye usafiri huo zimetokana na mchezo wa hovyo uliotaka kuchezwa na mwendeshaji wa mradi huo, lakini Serikali ilimshtukia.

Mradi huo ulionekana kuwa mkombozi wa gharama za usafiri kwa wananchi kutokana na kuwahi kufika ofisini au katika shughuli nyingine, nauli nafuu, usalama vituoni na ndani ya mabasi na utaratibu mzuri wakati wa kupanda ulisababisha hata wenye magari binafsi, kudiriki kuyaacha majumbani au kwenye maegesho karibu na vituo vya mabasi.

Lakini sasa, huduma hiyo imegeuka shubiri. Wizi uliokuwepo enzi za mabasi ya Uda pekee umerejea, msongamano ndani ya mabasi umerejea, uhakika wa usafiri si mkubwa kama ilivyokuwa awali na hakuna shaka kuwa baadhi ya walioamua kupumzisha magari yao binafsi sasa wameghairi, kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi wa hivi karibuni.

Akizungumzia mradi huo Kamwelwe alisema, “Wananchi watulie mambo mazuri yanakuja watafurahia haya yote ni matokeo ya mwendeshaji kutaka kuleta mchezo mchafu ambao Serikali tukasema hapana, maana alipewa muda halafu akataka kuingia moja kwa moja na kisha atutoe kabisa,”

“Nawaahidi kila kitu kitakuwa sawa mambo yanarekebishwa na usafiri utarudi katika hali ya kawaida na tutahakikisha kadiri tunavyoendelea haya mabasi yanafika hadi uwanja wa ndege.”

Hivi karibuni Mwananchi liliibua sakata la mabasi 70 yaliyoagizwa mahsusi kwa ajili ya mradi huo kukwama bandarini, huku uchache wa mabasi hayo ukitajwa kuwa chanzo cha foleni na usumbufu mbalimbali.

Septemba mwaka huu, akizungumzia suala la mabasi hayo ambayo hadi jana jioni yalikuwa bado bandarini, msemaji wa kampuni ya mabasi yaendayo haraka ya Udart, Deus Bugaywa alisema mabasi hayo yalizuiwa kutoka bandarini kusubiri kibali cha Dart.

Wakati Dart ikisema waendeshaji mradi huo hawajakamilisha taratibu zitakazowezesha kuyatoa mabasi hayo na kuyaingiza barabarani, Udart inasema imeshakamilisha taratibu zote na inachokisubiri ni ridhaa ya wamiliki wa mradi kauli inayofanya mabasi hayo kuendelea kuwepo bandarini kwa zaidi ya miezi minne.

Jana pia, Kamwelwe aliilalamikia benki ya uwekezaji ya Umoja wa Ulaya kukwamisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa viwanja vinne vya ndege nchini.



Chanzo: mwananchi.co.tz