Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri wa Dar kuelekea Morogoro, Dodoma majanga

35094 Pic+usaf Mabasi ya Kusafirisha Abiria

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamia ya wananchi wanaoelekea mikoa ya Morogoro na Dodoma kuanza muhula mpya wa masomo na kurejea kazini wamekwama katika stendi ya mabasi ya Ubungo jijini Dar es Salaam kutokana na kukosa usafiri.

Licha ya baadhi yao kufika mapema lakini walijikuta wakizidi kusota kadri muda ulivyokuwa ukienda huku wafanyakazi, wanafunzi wakionekana kuhaha zaidi.

Mwananchi lililofika kituoni hapo leo Jumapili Januari 6, 2019 na kuzungumza na baadhi ya wasafiri ambako mmoja wa wasafiri hao, Alexandra Petro akishangazwa na wingi huo wa abiria na kwamba licha ya wengi kufika saa 11 alfajiri lakini hadi saa 5 asubuhi walikuwa hawajapata usafiri.

"Kama unavyoona foleni ya hapa ilivyokuwa ndefu, tumezoea kuwa magari ya Morogoro ni mengi lakini hii ni tofauti. Nilikuwa ndani kila gari lililokuja niliambiwa limejaa hadi ikafika saa 2 ndiyo nikauliza ikoje nikaambiwa leo tiketi zinakatiwa ofisini," amesema Petro

Anasema kutokana na hali hiyo ilimlazimu kwenda kuangalia kama atapata tiketi katika ofisi za kampuni ya mabasi ya Abood ambapo aliambiwa tiketi zinazopatikana muda huo ni basi la saa 6 mchana.

Neema Kitandu ambaye ni mwalimu katika Shule ya Sekondari Kingorwila amesema mpaka sasa haoni dalili ya kupata usafiri kuelekea Morogoro, kubainisha kuwa ameamua kurejea nyumbani.

"Nimepanga foleni saa nzima sioni ikisogea nikakata tamaa nikarudi kukaa humu ndani nione kama nitapata usafiri mwingine lakini sioni dalili. Nitakata tiketi ya kesho asubuhi kabla ya kuondoka ili niwe na uhakika kuliko kufika usiku," amesema Neema.

Mmoja wa wanafunzi wanaosoma jijini Dodoma Lawrencia Mushi amesema haijawahi kutokea akapata adha ya usafiri kama leo tangu aanze kusoma jijini humo miaka mitatu iliyopita

"Kila siku huwa naondoka siku moja kabla ya kufungua shule lakini leo nimekwama na badala yake tiketi niliyoipata ni ya kesho saa sita mchana. Hata gari nililokata huwezi kuamini  sikuwahi kulipanda na huwa nalidharau sana lakini sina jinsi," amesema mwanafunzi huyo.

Wakala wa mabasi ya Shabiby Line yanayofanya safari zake kwenda Dodoma, Nahabu Chori amesema tiketi za magari hayo zilianza kuadimika wiki moja kabla ya Sikukuu ya Krismasi.

"Lakini hii hali kama imeongezeka kwa sababu zamani magari yalikuwa yanapishana saa moja katika muda wa kuondoka lakini hivi sasa kila baada ya nusu saa gari inatoka," amesema.

Amesema licha ya magari mengi kutoka lakini bado uhitaji ni mkubwa jambo ambalo linafanya baadhi ya watu kusubiri hadi siku moja.

"Kwa mfano hizi tiketi tunazokatisha hapa ni za kesho kutwa, magari ya kesho yote yamejaa na kutokana na hali hiyo kuna mtu ameridhia kulipia nauli ya Dodoma ili afike Morogoro," amesema Chori.

Mwananchi pia ilifika ofisi za mabasi ya First Choice yanayofanya safari zake kuelekea Dodoma na kukuta nafasi tano pekee ndizo zilizobakia katika gari ya mwisho kesho huku katika ofisi za Kimbinyiko tiketi zinazopatikana ni za keshokutwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz