Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri mwendokasi D’Salaam unavyowaliza wananchi

45546 Pic+mwendokasi Usafiri mwendokasi D’Salaam unavyowaliza wananchi

Sat, 9 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) ulipoanza miaka mitatu iliyopita, wakazi wa Dar es Salaam walikuwa na matumaini utatatua changamoto za usafiri zilizokuwa zikiwakumba kutoka ama kwenda katikati ya jiji hadi Kimara na Morocco.

Mei 2016, ulipozinduliwa ulikuwa na utaratibu mzuri kuanzia ukatishaji wa tiketi, kupanda ndani ya mabasi yalikuwa ya kutosha huku yakifika vituoni kwa wakati, hivyo abiria walikuwa hawakai muda mrefu vituoni.

Hata hivyo, kadri siku zinavyokwenda wasafiri wanakata tamaa kuhusu usafiri huo kwa namna unavyoendeshwa. Baadhi ya wananchi wanaoutumia wameliambia Mwananchi kuwa mradi huo kwa sasa si mkombozi tena, bali ni kero kutokana na adha wanazozipata.

Mkazi wa Ubungo, Anna Richard alisema jana kuwa, wakati mradi huo unaanza kulikuwa na utaratibu wa kukata tiketi za kielektroniki kisha kuzipitisha kwenye mashine maalumu kabla ya kuingia kituoni ambao hivi sasa haupo, badala yake wapo watu wanaokatisha tiketi hizo. Mkazi wa Shekilango, Aloyce Paul alisema imekuwa kawaida mtu anayeishi Manzese kupanda basi linalokwenda Ubungo au Kimara, na kugeuza nalo ili apate unafuu kufika mjini.

Paul aliziomba mamlaka husika kuweka mazingira bora ya uendeshaji na kuongeza mabasi kwa kuwa yaliyopo hayatoshelezi kulingana na mahitaji hasa baada ya baadhi ya daladala kusitishiwa leseni za kusafirisha abiria kwenda mjini.

Kwa upande wake, Julius Mapo alisema hivi sasa mtu akipanda basi ni nadra kusikia vituo vikitangazwa kupitia vipaza sauti vilivyomo ndani ya magari hayo tofauti na awali. “Kutotangazwa vituo kunasababisha usumbufu kwa baadhi ya watu hasa wenye ulemavu wa macho, ni vyema mamlaka husika zikarekebisha changamoto hii na nyingine,” alisema Mapo.

Akizungumzia hali hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alikiri kuwapo kwa upungufu wa mabasi akisema imesababishwa na kuharibika kwa magari 40.

“Baada ya kuona hali hii niliamua kuagiza wasaidizi wangu kuingilia kati ili mabasi haya yatengenezwe kwa wakati. Ninavyozungumza na wewe tayari baadhi yameshaanza kurudi barabarani, changamoto zingine ulizonieleza nitazifuatilia kwa ukaribu,” alisema Jafo.



Chanzo: mwananchi.co.tz