Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri bado mwiba Dar, Moshi

35181 Pic+moshi Usafiri bado mwiba Dar, Moshi

Tue, 8 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Moshi. Wakati muhula mpya wa masomo kwa shule za msingi na sekondari ukianza leo, baadhi ya wanafunzi, walimu watashindwa kuhudhuria vipindi kutokana na kukosa usafiri.

Wanafunzi wanaotokea Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali hususani Morogoro, Dodoma na Tanga jana walijikuta njia panda kutokana adha ya usafiri waliyokutana nayo Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo.

Mwandishi wetu alikishuhudia foleni za abiria wakikata tiketi bila kujali jua kali lililokuwa likiwaka mchana.

Mmoja wa wasafiri hao, Alexander Petro alishangazwa na wingi huo wa abiria akisema licha ya wengi kufika saa 11 alfajiri, hadi saa tano asubuhi walikuwa hawajapata usafiri.

Neema Kitandu ambaye ni mwalimu katika Shule ya Sekondari Kingolwira alisema licha ya kufika mapema, hapakuwa na dalili ya kupata usafiri wa Morogoro hivyo kuamua kurejea nyumbani.

“Nimepanga foleni saa nzima sioni ikisogea nikakata tamaa nikarudi kukaa humu ndani nione kama nitapata usafiri mwingine lakini sioni dalili. Nitakata tiketi ya kesho asubuhi ili niwe na uhakika kuliko kufika usiku,” alisema Neema.

Mmoja wa wanafunzi wanaosoma Dodoma, Lawrencia Mushi alisema hajawahi kupata adha ya usafiri kama jana tangu aanze kusoma huko miaka mitatu iliyopita.

“Kila siku huwa naondoka siku moja kabla ya kufungua shule lakini leo (jana) nimekwama. Tiketi niliyoipata ni ya kesho saa sita mchana. Hata gari nililokata huwezi kuamini sikuwahi kulipanda na huwa nalidharau sana lakini sina jinsi,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria, (Chakua), Hassan Mchanjama alisema kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaohitaji kurudi shuleni kwa ajili ya muhula mpya wa masomo unaoanza leo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanaendelea kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kasi kulingana na ongezeko la abiria waliopo stendi hapo.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu aliiomba Sumatra kuongeza mabasi ya ziada ili kukidhi mahitaji.

Hata hivyo, viongozi wa Sumatra hawakupatikana jana kuzungumzia adha hiyo na maombi hayo ya taboa baada ya simu za viongozi wake, mkurugenzi wa udhibiti wa barabara, Johansen Kahatano na ofisa leseni, Habiba Tambaza kuita bila majibu.

Imeandikwa na Aurea Simtowe, Fortune Francis (Dar) na Janeth Joseph (Moshi)



Chanzo: mwananchi.co.tz