Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri Moshi - Dar majanga, wasafiri watozwa nauli kubwa

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Baadhi ya daladala zinazofanya safari kati ya Mbagala na Gongo la Mboto, Dar es Salaam, jana zilisaidia kuziba pengo la uhaba wa mabasi katika stendi kuu ya mjini Moshi.

Daladala hizo zilipatiwa vibali vya muda Desemba, 2018 na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kwa ajili ya kusafirisha abiria kwa njia ya Dar es Salaam - Moshi - Arusha na Morogoro pamoja na Dodoma, lengo likiwa ni kupunguza adha ya usafiri kipindi cha mwisho na mwanzo mwa mwaka. Hata hivyo, jana, licha ya mabasi hayo kupunguza msongamano wa abiria waliofurika asubuhi kituoni hapo, mamia ya wasafiri waliendelea kufurika kutokana na wengi wao kuanza kurejea kwao hususan Dar es Salaam baada ya mapumziko ya sikukuu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi kituoni hapo, baadhi ya wasafiri walilalamikia kuuziwa tiketi kwa gharama kubwa ya kati ya Sh35,000 hadi Sh40,000 na kupewa tiketi zilizoandikwa Sh28,500.

Hadija Juma aliyekuwa akielekea Dar es Salaam alisema alifika kituoni hapo alfajiri, lakini aliuziwa tiketi kwa Sh32,000. Nauli halali ni Sh28,500.

“Wakati naingia kwenye gari nilikutana na watu wa ukaguzi, waliponihoji niliwaambia nimelipa Sh32,000 lakini tiketi iliandikwa Sh28,500, madalali waliposikia hivyo walinivuta na kunishusha kwenye gari kuhofia kukamatwa, hawa madalali hapa stendi wanatutesa kweli,” alisema Hadija.

Naye Haika Mtei alisema tatizo la kupandishwa kwa nauli ni kilio cha kila msafiri anayefika kituoni hapo na kushauri wasafiri wengine kuwa makini dhidi ya madalali hao.

“Hapa stendi tunanyanyasika kutokana na hawa madalali wanaotupandishia nauli ovyo, tunaiomba Sumatra ifanye kazi yake ipasavyo, tunawaona wafanyakazi wa Sumatra wapo wengi lakini tatizo linazidi kuwa kubwa,’ alisema Haika.

William Gano, wakala wa mabasi yaendayo Dar es Salaam alisema japokuwa abiria ni wengi, lakini hakuna atakayekosa usafiri isipokuwa tatizo kubwa kwa sasa ni wingi wa madalali wanaowalangua abiria kwa kuwauzia tiketi kwa bei ya juu.

Tajiri, Sumatra wanasemaje?

Mmiliki wa mabasi ya Ibra Line, Ibrahim Shayo alikiri kuwa madalali ni changamoto wanayokumbana nayo katika ukatishaji wa tiketi, lakini akawashauri abiria wakate tiketi kwenye ofisi za mabasi ili kuepuka kulanguliwa.

“Wasafirishaji tunakutana na changamoto kubwa, sisi tunatoza nauli halali ya Sumatra ya Sh28,500 kwa mabasi ya kawaida kwenda Dar es Salaam na yale ya semi luxury na luxury nauli yake ni Sh35,000 hadi Sh40,000, lakini hawa madalali wanakuja na bei zao halafu lawama zinarudi kwetu,” alisema Shayo.

Akizungumzia suala la madalali kupandisha nauli, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani Kilimanjaro, Johns Makwale alisema litamalizika endapo abiria watahamasika kukata tiketi kwenye ofisi za mabasi husika na kwa mawakala halali huku wakiachana na madalali.



Chanzo: mwananchi.co.tz