Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usafiri Dar-Moshi mbinde, Moshi-Dar Sh10,000

33156 Pic+usafiri Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Licha ya ongezeko la mabasi zaidi ya 182 yaliyopewa kibali cha kusafirisha abiria mikoani, hali ya usafiri katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam imezidi kuwa tete hivyo kuilazimu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), kutoa vibali kwa mabasi ya kati (abiria 28) ili kupunguza adha hiyo.

Hali ya usafiri imezidi kuwa ngumu kuelekea ni Sikukuu ya Krismasi kesho na ya Mwaka Mpya wiki ijayo.

Kinyume chake, idadi ya abiria wanaotoka katika baadhi ya mikoa kuelekea Dar es Salaam imepungua kiasi cha mabasi kupunguza bei ya nauli hadi Sh10,000.

Kwa siku tatu mfululizo, upatikanaji wa usafiri katika kituo hicho umekuwa mgumu na kusababisha kuwapo kwa vitendo vya utapeli na wizi kwa wanaotaka kusafiri.

Lakini wakati hali ikiwa tete Ubungo, abiria waliokuwa wanasafiri kutoka Moshi kwenda Dar es Salaam, jana walikuwa wanachekelea baada ya nauli kushuka kutoka Sh32,800 hadi Sh10,000 kutokana na mabasi kukosa abiria.

Lakini si wote wanaosafiri kwa ajili ya mapumziko. Mmoja wao ni Rajabu Mruma ambaye alisema alitaka kwenda Same kwenye msiba wa shangazi yake lakini amekosa usafiri kwa siku ya pili.

“Jana (juzi) nilifika hapa nikakosa usafiri. Leo (jana), toka saa 11 alfajiri nimekuja hakuna gari wala tiketi sijui kama nitafanikiwa kwenda kuzika kesho (leo),” alisema Mruma.

Mwingine ni Irene Mkonyi aliyekuwa anampeleka mdogo wake Hospitali ya Rufaa KCMC ambaye alisema amekaa kwa saa zaidi ya tano bila kupata usafiri.

Mkurugenzi wa usafiri na udhibiti wa barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema kinachochangia kukosekana kwa usafiri ni idadi kubwa ya abiria kukata tiketi dakika za mwisho.

Alisema wameruhusu mabasi madogo kusafirisha abiria lakini bado wanaendelea kuhimiza wamiliki wenye mabasi kuyapeleka yakakaguliwe na kupewa vibali.

Alisema abiria walioongezeka ni wa mikoa ya Morogoro, Tanga Kilimanjaro na Arusha na kusemsa jitihada za kukabiliana na changamoto hiyo zinaendelea.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Enea Mrutu alisema chanzo cha adha ya usafiri ni pamoja na kushikiliwa kwa mabasi manane eneo la Mkata yakielekea Dar es Salaam.

Lakini kuhusu hilo, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Bararabarani, Fortunatus Muslimu alisema hafamu chochote waulizwe Sumatra.

Kahatano alipoulizwa kuhusu hilo alisema hajapata taarifa za kuzuiwa kwa mabasi hayo huku akisisitiza kwamba abiria wote waliotaka kusafiri leo waliondoka.

Mmoja wa madereva wa mabasi yaendayo mikoani, Omari Hamza alisema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa abiria wanaorudi jijini Dar es Salaam kiasi cha baadhi ya mabasi kurudi matupu kabisa bila abiria.

Mmoja wa viongozi wa Stendi ya Mabasi Moshi, Aloyce Ndanu alisema mabasi mengi ya nyongeza yaliyoelekezwa na Sumatra kusafirisha abiria mkoani Kilimanjaro yamesaidia nauli kushuka. Mkoani Manyara, abiria ambao hutumia mabasi yanayoanzia safari zake mjini Moshi na Arusha kwenda mikoa ya Kati na Kanda ya Ziwa walikwama kutokana na mabasi hayo kufika Babati yakiwa yamejaa.

Wakala wa mabasi, Godfrey Maasay alisema yapo mabasi machache yanayoanzia safari zake Babati.



Chanzo: mwananchi.co.tz