Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upungufu wa malisho chanzo cha migogoro ya ardhi

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Upungufu wa maeneo ya kuchungia umesababisha wafugaji kuhamahama kutafuta malisho na wakati mwingine kulisha kwenye maeneo yasiyostahili na hivyo kuleta migogoro ya ardhi.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Machi 18, 2019 na kaimu mkurugenzi wa idara ya uendelezaji wa malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo, Dk Asimwe Rwiguza wakati akifungua mkutano wa siku ya nyanda za malisho ulioandaliwa na chama cha nyanda za malisho nchini.

Dk Rwiguza ambaye alimwakilisha waziri wa mifugo na uvuvi, Luhaga Mpina katika mkutano huo, amesema migogoro mingi imekuwa baina ya wafugaji na wakulima, hifadhi za Taifa, kampuni za ranchi za Taifa na jamii zinazozunguka wafugaji.

Hata hivyo, amesema Serikali imekuwa na jitihada mbalimbali katika kuongeza upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo kwa kutenga fedha kwa ajili ya kupima na kutenga maeneo ya malisho.

Amesema uhaba wa malisho umeifanya Serikali kufikiria kutenga maeneo kwa ajili ya kusaidia wafugaji ambapo katika mwaka 2018/2019 iliainisha hekta 350,576 kwa ajili ya maeneo ya malisho yaliyotengwa kutoka katika maeneo ya wizara na taasisi zake.

Aidha amesema kumekuwa na ongezeko la mimea vamizi katika maeneo mbalimbali ya kuchungia na kukosekana kwa lishe bora kwa mifugo na kupunguza tija ya uzalishaji katika sekta ya mifugo.

Naye mwenyekiti wa chama cha nyanda malisho Tanzania (RST), Dk Ismail Selemani amesema maisha ya Watanzania wengi yanategemea rasilimali zinazopatikana katika nyanda za malisho hasa malisho ya mifugo na wanyamapori wanaopatikana katika nyanda hizo.

Dk Selemani amesema Tanzania ni moja ya nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya mifugo barani Afrika ambayo inategemea uhai wa nyanda za malisho.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha wanafunzi wanaosoma masuala ya nyanda za malisho, John Bosco Patrick amesema lengo la kuanzisha chama hicho ni kuwaunganisha wanafunzi wa kozi hiyo ili waweze kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo hasa tasnia ya malisho nchini.

Pia amesema ipo changamoto ya kutotambulika kwa tasnia hiyo katika muundo wa ajira serikalini, kwani hadi sasa wanaopata ajira serikalini wanaajiriwa kama wataalamu wa mifugo na si wataalamu wa nyanda za malisho na hivyo kushindwa kuitumia taalamu yao vizuri.



Chanzo: mwananchi.co.tz