Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upungufu vyumba vya maabara unavyozitesa shule za sekondari -3

60057 NYUMBAPIC

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki iliyopita tuliangalia upungufu katika wilaya zote nchini, wiki hii tutaangalia hali ilivyo shuleni katika wilaya ya Lushoto ambayo ina upungufu zaidi wa maabara. Sasa endelea...

Kilomita nane kutoka Lushoto mjini ndipo ilipo shule ya Sekondari ya Prince Claus. Shule hii ilianzishwa mwaka 2010.

Shule ina majengo matatu yaliyoungana. Upande mmoja kuna jengo moja ambalo halijakamilika na ndani linatumika kama jiko. Jengo hili ambalo lina uwazi mkubwa sio kama darasa la kawaida, limejengwa kwa matofali ya kuchoma, halina sakafu, madirisha wala milango ikiashiria bado lilikuwa linaendelea kujengwa ila ujenzi ulisimama muda kidogo.

Upande wa kushoto wa jengo hilo kuna majengo mengine yaliyoungana kama matano. Upande mmoja yalikuwapo mawili yaliyofuatana yenye ukubwa uliolingana na ule wa jengo la mwanzo. Tofauti ya majengo hayo na lile la mwanzo, haya yalikuwa yamesakafiwa vizuri licha ya kuwa hayakuwa na madirisha na milango.

Paa lake lililokuwa halikumaliziwa kofia za katikati kwenye baadhi ya maeneo, lilionyesha kuwa lilikuwa ni la muda mrefu kidogo ikiwa na maana kuwa ujenzi wake umesimama siku za karibuni.

Chumba cha tatu baada ya majengo yale mawili ni ofisi ya walimu. Upande mmoja kulia mwa mlango, kuna meza ndefu iliyokuwa na mfumo wa maji katikati, na pembeni kulikuwa na makabati ya ukutani.

Pia Soma

Meza hiyo ilijaa vifaa mbalimbali vya maabara na vingine vikikwa chini, katika makabati yale kunaonekana chupa kama za dawa.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Yona Ndekiwa anafafanua kuwa meza ile ndogo ni maabara ya mfano ambapo wanafunzi wanapohitaji kufanya mazoezi kwa vitendo huchukua vifaa wanavyohitaji na kuvitumia kujifunzia katika darasa moja.

“Majengo matatu uliyoyaona ndio tunategemea kuwa ya maabara, lakini kwa kuwa hayajakamilika tunatumia darasa mojawapo kulingana na mahitaji,” anasema.

Anaeleza kuwa ujenzi wa maabara unategemea nguvu za wananchi na majengo hayo ya maabara yalianza kujengwa mwaka 2014, lakini mpaka sasa hayajakamilika kutokana na nguvu ndogo ya wazazi.

Hali hiyo haitofautiani sana na ile iliyopo katika Shule ya Sekondari Lushoto ambayo ina jengo moja la maabara lililokamilika na mengine mawili ambayo hayajakamilka yakiwa kwenye hatua ya kupigwa bati.

Licha ya chumba na maabara kutokuwa na mfumo wa maji na umeme, mwalimu mkuu wa shule hiyo Agness Shekuamba ambaye pia ni mwalimu wa somo la baiolojia, anasema kwa sasa wanalazimika kutumia chumba kimoja japo hakijakamilika kwani vingine viwili bado vina hatua kubwa mpaka kukamilika.

Katika shule ya Shambalai ambayo ni miongoni mwa shule kongwe wilayani humo, hali haikuwa tofauti, kulikuwa na chumba kimoja cha maabara kilichokamilika na vingine viwili ambavyo vimefikia hatua ya kupauliwa.

Uchunguzi wa gazeti hili baada ya kutembelea baadhi ya shule ulibaini kuwa nyingi zina majengo yaliyoanza kujengwa lakini bado hayajakamilika, vilevile majengo hayo yalianza kujengwa miaka ya 2014-2015 kutokana na agizo la Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete lakini mpaka sasa mengi hayajakamilika.

Changamoto nyinginezo

Baada ya kutembelea baadhi ya shule wilayani humo, Mwananchi lilibaini changamoto nyingine ni uhaba wa vifaa vya kufanyia mazoezi hayo.

Mwalimu Haji Muhidini ambaye anafundisha somo la kemia, anasema kuna changamoto ya miundombinu ya kuhifadhia vifaa vichache vilivyopo na mazingira yasiyo rafiki ya kufundishia.

“Maabara yetu kama ulivyoiona haina ‘shelf’ (makabati) ya pembeni kwa ajili ya kutunzia vifaa, mfumo wa maji wala umeme. Lakini kule kwenye kuhifandhia zile kemikali tunaweka kwenye kabati au boksi hivyo inakuwa sio rahisi kuendelea kuwa na ubora wake kwa muda mrefu,” anasema.

Kwa upande wake Mwalimu Bethinasia Hena anayefundisha hesabu na fizikia, anasema wingi wa vipindi pia ni changamoto kubwani.

Chanzo: mwananchi.co.tz