Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upofu umeshindwa kuzima ndoto za wanawake hawa

48381 PIC+UPOFU

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tofauti ya wanawake hawa watatu; Neema, Nuru na Lucy na wewe unayesoma hapa ni kwamba makala haya hawataweza kuyasoma bila usaidizi wa watu wengine. Wao hawaoni. Neema alipoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka 22, Nuru akiwa na miaka 17 na Lucy wakati akiwa na miaka 24.

Pamoja na kuwa wamepoteza uwezo wa kuona, lakini wanayoyafanya yanastahili kuandikwa ili yabaki katika kumbukumbu kama ilivyo kwa mashujaa wengine.

Ulemavu siku zote huhusishwa na kushindwa, kutojiweza au kutegemea kusaidiwa katika kila kitu kwenye maisha. Lakini Nuru, Neema na Lucy wanathibitisha kuwa dhana hiyo haina ukweli wowote. Pamoja na kukosa uoni, wamekuwa wakijishughulisha katika ujenzi wa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Neema Mahonya, binti mwenye umri wa miaka 28, anaeleza safari yake ya miaka sita bila kuona chochote. Alizaliwa akiwa anaona na kupata elimu ya msingi na sekondari. Ndoto yake ya kufanya kazi kama mtaalamu wa masuala ya bahari ilikatika ghafla akiwa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Uvuvi Mbegani kilichopo Bagamoyo, Pwani.

Akiwa nyuma ya cherehani akiendelea kushona gauni, Neema ambaye sasa anafanya shughuli zake ndani ya viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam anasema maisha yake ni mazuri kwani mbali na kushona, hujishughulisha na biashara nyingine za kutengeneza mazulia, ubuyu na karanga.

“Ilinichukua muda kukubali kuwa sitaona tena na maisha inabidi yaendelee. Namshukuru Mungu sasa naendelea na maisha na kwa kiasi kikubwa ninajitegemea kwa kila kitu.

Mpenzi huyo wa muziki wa injili na Bongo Fleva, anasema wapo wasanii wengi anawapenda lakini kwa bahati mbaya hajawahi kuwaona kwa kuwa wakati wanaanza kupata umaarufu alikuwa ameshapoteza uwezo wa kuona.

“Zaidi huwa nasikiliza redio na bahati nzuri najua sauti za karibu watu wote maarufu na muhimu, kwa mfano nikisikia sauti najua huyo Rais Magufuli au Lowassa (Waziri mkuu wa zamani). Hata Spika wa Bunge (Job Ndugai) naijua sauti yake ila sura yake siifahamu,” anaeleza.

“Diamond, Lady Jay Dee nawajua sura zao, ila kuna wanamuziki nawapenda sijui wanafanana vipi kama Nandy, Harmonize, Harmorapa na mwanamuziki ninayempenda sana Angel Benard.”

Anafanyaje kazi zake ikiwa analazimika kupangilia rangi, kutumia sindano au kuchagua uzi unaoendana na vitambaa anavyoshona? “Kuna wakati nahitaji usaidizi wa kufahamu tu rangi ya vitambaa vya mteja, ninachofanya nauliza tu hiki kina rangi gani, nikishajua basi nafahamu rangi ya uzi ninaotakiwa kutumia. Nyuzi zangu zote nimeziweka alama, nikigusa tu najua huu wa rangi gani,” anasema.

Neema anajinasibu kuwa anaifahamu cherehani nje ndani.

“Hata ikikwama kidogo najua wapi imekorofisha, kama naweza kurekebisha nafanya hivyo, kama siwezi namuelekeza mtu anisaidie kuparekebisha.”

Anapomaliza kushona nguo, jioni hutumia muda wa ziada kutengeneza mazulia ya mlangoni ambayo hutumia vitambaa vilivyobaki na pia mwishoni mwa wiki hutengeneza ubuyu ambao huuza jumla na rejareja.

Ukikutana na Nuru Awadhi, diwani wa viti maalumu Wilaya ya Ilala kitakachomtofautisha ni miwani myeusi ambayo huivaa muda wote. Ni mrembo ambaye wakati wote huvalia nguo nadhifu na vito.

Mwonekano wa Nuru unavutia, mavazi yake yamepangiliwa kwa namna ya kuwafanya wanaopita karibu yake wageuze shingo.

“Siioni dunia, lakini kila nikiamka asubuhi huwa najikumbusha kuwa dunia inaniona, ndio maana mwonekano ni kila kitu kwangu, napenda kupangilia vizuri mavazi yangu,” anasema.

Anasema huenda mbali zaidi kuhakikisha anaonekana vizuri kwa kuwashirikisha watu wake wa karibu au hata kuwapigia simu wanamitindo.

“Kwa mfano ninaweza kuwa na nguo mpya sijui nivae na kilemba cha aina gani, huwa nampigia simu Martin Kadinda (mbunifu wa mavazi) kumuomba ushauri juu ya nguo ninazotaka kuvaa katika siku husika.”

Mwanamama huyu anajipenda lakini moja ya ndoto zake ni kuona watu wenye ulemavu wote wakiwa na mwonekano nadhifu ili kuondoa dhana kwamba wao ni watu wasiojiweza.

“Huwa ninawakumbusha wenzangu siku zote ni lazima tujipende, sisi hatuwaoni lakini wapo watu wanaotuona na tunapokuwa katika mwonekano usiovutia huwafanya watudharau au kututenga,” anafafanua.

Mshindi huyo wa tuzo mbili za I Can zilizotolewa hivi karibuni na mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, pamoja na ulemavu wake amekuwa akijitolea kuisaidia jamii kwa hali na mali.

“Kuna wakati kama kiongozi inabidi nisaidie jamii yangu hata kama wanahitaji pesa inabidi nitumie zangu binafsi, hata kama kidogo inabidi nijitoe.”

Nuru pia amekuwa akiwasaidia watu wenye ualbino kwa kuwapa mafuta maalumu ili kuwakinga na miale ya jua ambayo huwasababishia saratani ya ngozi.

Kwa Lucy Mgombere, mambo ni magumu zaidi kwa sababu licha ya kupoteza uoni, hasikii vizuri hivyo kufanya mawasiliano kwake kuwa magumu.

Hata hivyo, kushindwa kuona na kusikia vimeshindwa kuzima ndoto zake za kuwa mpika batiki na mtengeneza sabuni mashuhuri.

Anajinasibu kuwa nguvu ya macho imehamia katika hisia inayomfanya awe mbunifu katika uchanganyaji wa rangi kwenye batiki.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32, kila wiki hupanda daladala mara moja kutoka kwake Mabibo mpaka soko la Karume, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kununua majora (vitambaa) ya kutengenezea batiki.

“Ninabeba tape (kifaa cha kupimia urefu wa vitambaa) yangu, ninakwenda dukani kununua vitambaa na rangi kama nimeishiwa, kila rangi ninapopewa huwa ninaiweka alama palepale ili nisichanganye,” anasema.

“Rangi zangu zote nazijua kwa alama ninazojiwekea kwa kuzifunga nyuzi, upana wa uzi ndio unanitambulisha rangi.”

Anasema ulemavu walionao huwafanya wawe watu wenye mpangilio zaidi katika maisha.

“Kwa mfano, wewe (mwandishi) unaweza kuweka mswaki wako popote kwa sababu ukiutaka unaweza kupekua huku na kule, mimi nisipouweka mahali maalumu itabidi nisaidiwe kuupata,” anasema.

Hata hivyo, anasema zipo changamoto za hapa na pale hasa katika vyombo vya usafiri ikiwamo kupigwa vikumbo kwenye daladala na kushindwa kusikia ipasavyo vituo vinapotangazwa, lakini hazijawahi kumfanya ajisikie tofauti au zimkatishe tamaa.

“Najua kila mtu amepewa uwezo fulani au kunyimwa kitu maishani, hainiumizi pale ninapokutana na changamoto kutokana na kushindwa kuona au kusikia, siku zote najipa moyo kwamba kuna kitu Mungu amenipendelea.”



Chanzo: mwananchi.co.tz