Zaidi ya familia 35 za mtaa wa Kinengene kata ya Chikonji Manispaa ya Lindi hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuezuliwa na upepo huku nyingine zikianguka.
Nyumba za kaya hizo zinazokadiriwa kuwa na watu 135 zimeezuliwa baada ya mvua iliyoambatana na upepo kunyesha katika kata hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi iliyofika kwenye eneo hilo, baadhi ya wananchi wa mtaa huo wamesema mvua hiyo iliyoanza kunyesha Januari 15, 2022 imesababisha kuharibu makazi na vitu mbalimbali.
Diwani kata ya Chikonji Abedi Bakari amesema katika mtaa wa Kinengene nyumba zimeharibika, ghala moja la mazao pamoja na jengo la kituo Cha afya limeezuliwa.
Mwenyekiti wa ACT Mkoa wa Lindi, Isihaka Mchinjita amesema uharibifu ni mkubwa hasa makazi ya watu hivyo ni vyema uongozi na wadau wasaidie familia hizo kupata mahitaji muhimu ya chakula na malazi.
Mchinjita amefika kwenye eneo hilo pamoja na baadhi ya wanacham,a wa chama hicho kutoa msaada kwa waathirika amesema kuwa msaada wa haraka unahitajika kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi hao ili kuwanusuru na magonjwa ya mlipuko.
“Sisi kama chama tumeguswa na tukio hili tumeona vyema kuja kuwafariji waathirika wa mvua hizi kwa kuleta unga, sukari na maharag” amesema Mchinjita.
Asha Malima ambaye ni miongoni mwa familia zilizokosa makazi amesema mvua hiyo ilikuwa na upepo mkali imeharibu kila kitu kilichokuwa ndani na kuomba Serikali na wasamaria wema wawasaidie ili waweze kujikimu kimaisha.