Upepo mkali uliombatana na mvua kubwa umebomoa na kuharibu nyumba 43 katika Kijiji cha Mambamba na Majengo Kata ya Mndumbwe pamoja na chumba kimoja cha darasa la Shule ya Msingi Namkomolela iliyopo kata ya Milongodi wilayani humo.
Akizungumza leo Jumatatu Novemba 21, 2022 mara baada ya kutembelea wananchi walipatwa na madhara hayo, Katibu Tawala Wilaya ya Tandahimba Juvenile Mwambi akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya maafa wametoa pole kwa wananchi wa vijiji vya Mambamba, Majengo na Namkomolela walioathirika na uharibifu huo.
Amesema mvua iliyoleta madhara ilinyesha Novemba 15, 2022 na kusababisha athari kwa wakazi wa vijiji hivyo.
“Hii mvua imeleta madhara makubwa kwenye nyumba na makazi ya watu
ambapo nyumba 43 zimepata madhara sasa tunafanya tathmini ili kujua
ukubwa wa tatizo,” amesema Mwambi
Hata hivyo, baadhi ya waathirika Hassan Juma, mkazi wa Mambamba
alipotembelewa katika maeneo yao alisema tumepata madhara makubwa
kutokana na mvua na upepo mkali hivyo wanaimani kamati ya maafa itawasadia.
“Tunashukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake, kujali wananchi wake
kwa kufika na kuona hali halisi iliyojitokeza baada ya kupatwa na
maafa tumeathirika kwa kiasi kikubwa yaani hata vyakula vimelowa,
malazi hatuna lakini tunaimani na serikali yetu itatusaidia,” amesema
Juma.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya
Tandahimba, Robert Mwanawima amewahikikishia wananchi walioathirika na mvua katika Kata ya Mndumbwe na Milongodi kuwa Serikali ipo pamoja nao na hatua za awali zimechukuliwa.