Dar es Salaam. Alikuwa rafiki wa kweli. Ndivyo unavyoweza kusema ukiwazungumzia baadhi ya wakazi wa mtaa wa Tabata Kisiwani jijini Dar es Salaam waliobeba jeneza la Emmanuel Cosmas umbali wa zaidi ya mita 800 kabla ya kulipakia kwenye gari kwenda Kilosa, Morogoro kwa mazishi.
Wamesema wameamua kumsindikiza rafiki yao kwa miguu kutoka kanisani hadi eneo la Tabata Relini maarufu Tabata Mwananchi ambako kulikuwa na magari yanayokwenda Morogoro.
Kitendo hicho kilizua sintofahamu kwa kuwa baadhi ya watu waliopisha nao walidhani kuna mgogoro wa kifamilia.
Wakizungumza na Mwananchi, wakazi wa mtaa huo wamesema walimpenda mwenzao kwa sababu alikuwa mnyenyekevu na alipenda zaidi kusaidia watu.
“Emmanuel alikuwa kama familia, nyumbani kwangu ilikuwa kama kwake. Alikuwa akitusaidia mimi na wapangaji wenzangu kazi ndogondogo kwa malipo ambayo hakuwahi kupanga, aliridhika na kiasi chochote,” amesema mkazi wa mtaa huo, Alex Malanga.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Tabata Kisiwani, Rajabu Chala amesema hakukuwa na tatizo lolote bali vijana wenzake wametaka kumbeba rafiki yao kipenzi ambaye waliishi naye vizuri. Amesema alifariki dunia Februari 4, 2020.
Pia Soma
- Umoja wa Mabunge duniani watoa tamko zito sakata la Lissu
- Magoti wa LHRC afikisha siku 154 mahabusu
- Mtoto mchanga agundulika na virusi vya corona
Japhet Kanyika, rafiki wa karibu wa marehemu amesema alikuwa akisumbuliwa na ngiri kwa muda mrefu na alifanyiwa upasuaji.
“Hapa Dar es Salaam hakuwa na ndugu yoyote, amekuwa akiishi mwenyewe. Anapendwa sana na watu ndiyo maana unaona umati huu wote wamekuja hapa kumuaga,” amesema kijana huyo.
Kijana mwingine, Ramadhan Adam amesema marehemu alikuwa akifahamika kama “Rais” kwa sababu ni mtu wa watu, anapendwa na watu wote, watoto kwa wakubwa. Amesema hajawahi kusikia amepigana na mtu.