Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelekaji umeme vijijini washika kasi

036418103981aef4d8ce018fae2bc0b1 Umeme

Thu, 16 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAZI ya kupeleka umeme vijijini imeshika kasi huku Rais John Magufuli akihakikishia umma kwamba serikali yake itakapopewa ridhaa ya kuongoza tena haitashindwa kuvipatia vijiji vyote umeme.

Katika kudhihirisha nia hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema serikali haitasita kusitisha mkataba wa mkandarasi atakayeonekana kusuasua katika kutekeleza majukumu yake na kwenda kinyume na mkataba wa kazi ya kusambaza umeme.

Juzi akiwa katika kijiji cha Kenswa Nsimbo kilichopo kata ya Katumba wilayani Mpanda katika Mkoa wa Katavi, Mgalu alisema serikali haipo tayari kurudishwa nyuma katika juhudi zake za usambazaji umeme nchini.

Alisema serikali imesitisha mkataba wa mkandarasi wa mradi wa Wakala wa Umeme (REA) mkoani Mwanza kwa sababu ya kutotekeleza majukumu yake. Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mgalu, ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, jumla ya vijiji 10,446 vitakuwa vimesambaziwa umeme.

Aliwataka wakandarasi wote wa miradi ya Wakala wa Umeme (REA) kufanya kazi kwa bidii kufanikisha lengo hilo. Taarifa ya serikali inasema hadi Aprili mwaka huu, vijiji 9,112 kati ya vijiji 12,268 nchini, vilishafikishiwa umeme.

“Tumebakiza vijiji 3,156 tu. Tukichaguliwa hatuwezi kushindwa vijiji hivi vitatu tu,” alisema Rais Magufuli kupitia hotuba yake ya kufunga Bunge la 11 jijini Dodoma aliyoitoa mwezi uliopita.

Wizara ya Nishati inafafanua kwamba idadi hiyo ni sawa na ongezeko la vijiji 7,094 katika kipindi cha miaka mitano sawa na asilimia 287 ya vijiji vilivyokuwa na umeme mwaka 2015.

Mchanganuo wa wizara unaonesha jumla ya Wilaya na Halmashauri 36 za Tanzania Bara zimefikiwa na umeme katika vijiji vyake vyote huku kazi ya kuunganisha umeme kwa wateja ikiendelea katika wilaya hizo na nyingine.

Wilaya hizo ni Mafia, Isimani, Pangani, Rufiji, Chato, Bahi, Siha, Moshi, Hai, Mwanga, Rombo, Madaba, Buhigwe, Makambako, Korogwe Mjini na Mafinga.

Chanzo: habarileo.co.tz