Tarime. Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) , Joseph Nyamuhanga ametoa siku saba kwa uongozi wa Halmashuri ya Mji wa Tarime kutoa mchanganuo namna ambavyo zaidi ya Sh975 milioni zimetumika kwenye ujenzi wa jengo la utawala la halmshauri hiyo.
Nyamuhanga ametoa agizo hilo leo Juni 22,2019 baada ya kufanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi huo akisema hadi sasa kazi iliyofanyika haiendani na kiasi cha fedha kilichotolewa.
"Sasa hivi tunajenga vituo vya afya kwa Sh1.5 bilioni na kila kitu kinakamilika lakini ukiangalia hapa zimetumika karibia Sh1 bilioni ila kazi haiendani na thamani halisi ya fedha " amesema Nyamuhanga.
Nyamuhanga amesema kuwa amesikitishwa na kitendo cha halmashauri hiyo kushindwa kutuma Tamisemi mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo tangu alipotoa agizo la kufanya hivyo miezi sita iliyopita.
Amesema mbali na mchanganuo huo, pia mradi huo unatekelezwa taratibu na kuutaka uongozi wa halmashuri hiyo kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika na hatimaye kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Pia Soma
- Mghwira: Wafanyabiashara kuweni wabunifu
- Serikali ya Kenya kukagua wanaume kama wametahiriwa
- Kesi inayowakabili wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kampala Tanzania Julai 30
Akitoa taarifa za ujenzi wa mradi huo, Kaimu mhandisi wa halmashuri hiyo, Ngalula Tungu amesema mradi huo hivi sasa umesimama baada ya Serikali kuu kutokupeleka fedha zilizoombwa na mkandarasi kwa mujibu wa sheria na taratibu.