Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unyama! Majambazi wamuua baba yao kisha na wao kuuawa

Mauaji Abc.jpeg Wamuua baba yao kisha na wao kuuawa

Fri, 14 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu wawili wanaosadikika ni majambazi, wameuawa na wanakijiji baada ya kumuua kwa kumkata mapanga Mzee Ephraim Mavika (57) wakimlazimisha kuonyesha fedha.

Watu hao wameuawa katika Kijiji cha Wasa Wilaya ya Iringa na katika tukio hilo, wanafamilia sita wamejeruhiwa na majambazi hao ambapo mmoja wa aliyeuawa ni mtoto wa marehemu Mavika.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi (ACP) Allan Bukumbi, akizungumza na waandishi wa habari jana alisema tukio hilo lilitokea usiku baada ya vijana Matatizo Mavika na Christian Mavika kudaiwa kukodi majambazi kutoka Mafinga wilayani Mufindi ili kutekeleza uvamizi huo.

Bukumbi alisema vijana hao walifanya uvamizi huo  baada ya kupokea taarifa zisizo sahihi kuwa Mzee Mavika ametumiwa kiasi kikubwa cha fedha na mtoto wake, Tedy Mavika, anayeishi Dar es Salaam.

Alisema  watu hao waliwavamia wanafamilia hao wakiwa na silaha za jadi zikiwamo mapanga na nondo.

Wakati wa uvamizi huo, alisema  wanakijiji walipata taarifa na kwenda eneo la tukio na katika purukushani kati ya wavamizi hao na wanakijiji, wahalifu wawili kati ya saba walijeruhiwa na kufariki dunia.

Kamanda Bukumbi aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Matatizo Mavike, mkazi wa Wasa na Baraka Nyakunga, dereva bodaboda mkazi wa mtaa wa Balali Mafinga, wilayani Mufundi.

Pia, alisema watuhumiwa wawili ambao ni Hassan Mkalava, mkazi wa Ifunda na Christian Mavika, mkazi wa Ikugwe, Wasa, walikamatwa baada ya polisi kufanya msako na walipohojiwa walikiri kushiriki katika tukio hilo la uvamizi na mauaji.

Aidha, pikipiki mbili ambazo zilitumiwa na wahalifu hao zimekamatwa ambazo zina namba za usajili MC 578 DME rangi nyeusi na nyingine isiyokuwa na namba yenye injini namba KL162MJ rangi nyekundu zote ni aina ya King Lion.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live