Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ummy awaonya wakurugenzi

46f0a58e8b7cf68a939dc6e872f84c36 Ummy awaonya wakurugenzi

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu amesema hatamvumilia mkurugenzi wa halmashauri yoyote ambaye hatatenga asilimia 40 ya fedha za ndani kwa ajili ya maendeleo.

Alitoa onyo hilo wakati akizungumza na wakuu wa idara katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma juzi. Alisema suala la kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo ya halmashauri ni la kisheria.

Ummy alizitaka halmashauri zote kuhakikisha asilimia 40 ya fedha za maendeleo zinapewa kipaumbele katika kutekeleza miradi ya afya.

Aidha, alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Athuman Masasi kuhakikisha mapato yaliyoainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa hayapelekwi benki yanapelekwa ndani ya siku tatu.

Aidha, amezikumbusha sekretarieti za mikoa kutimiza majukumu yao ya kuzishauri halmashauri hasa katika ukusanyaji na matumizi ya mapato katika serikali za mitaa na kujenga utamaduni wa kuzitembelea na kufanya tathmini ya mambo waliyopanga.

Waziri huyo pia aliwataka watendaji wa halmashauri zote kushirikiana katika suala la ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi. “Watendaji wa halmashauri muache tabia ya kuwadharau na kupuuzia ushauri wa wanasiasa hususani madiwani.”

“Kuna baadhi ya watendaji wamekuwa wakipuuzia, kudharau na kutotekeleza ushauri wa wanasiasa wanapowashauri katika mambo mbalimbali ya kiutendaji ikiwamo suala la vyanzo vya mapato,” alisema na kuongeza:

“Nitoe wito kwa halmashauri zote nchini kuacha mara moja tabia ya kuwadharau wanasiasa kwa kudhani madiwani wote ni darasa la saba, sasa hivi kuna madiwani wana PhD na hata kama darasa la saba hao wamechaguliwa na wananchi na wanajua mambo mengi sana yanayohusu wananchi kwa sababu ndio wanaoishi nao,” alisema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema pamoja na kuwapo kwa mikakati mingi, wilaya ya Chamwino imekuwa haifanyi vizuri katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya serikali

Chanzo: www.habarileo.co.tz